IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Utumizi wa uwezo na fursa adhimu za bahari uwe ni utamaduni wa watu wote

7:31 - November 29, 2022
Habari ID: 3476166
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amiri Jeshi wa Vikosi Vyote vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametilia mkazo kubadilishwa kuwa utamaduni wa watu wote nchini utumiaji uwezo na fursa adhimu za bahari zilizopo.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Amiri Jeshi wa Vikosi Vyote vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa sisitizo hilo Jumatatu mjini Tehran katika kikao na baadhi ya makamanda wa jeshi la wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika mkutano huo ambao ulifanyika kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi la Wanamaji inayoadhimishwa tarehe 7 Azar, Ayatullah Khamenei ametoa wito wa kustawishwa katika pande zote uwezo wa upiganaji na wa zana za ulinzi katika Jeshi la Wanamaji na kuendelezwa uchukuaji hatua, ikiwemo upelekaji vyombo vya baharini kwenye maji ya mbali na ya kimataifa na akasema: kuimarishwa mawasiliano kati ya vikosi vya ulinzi na serikali na mihimili mingine ya dola kutasaidia katika kujenga maelewano, ushirikiano na ufanikishaji kazi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria historia ya safari za ubaharia za Wairani katika zama za nyuma ambazo zilipelekea kuenezwa utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu na wa Iran katika maeneo mengine ya dunia na akasema: licha ya historia hiyo na kuwepo fukwe ndefu za bahari kaskazini na hasa kusini mwa Iran, utamaduni wa kutumia fursa za bahari umesahaulika nchini na inapasa ubadilishwe kuwa utamaduni wa watu wote.

Ayatullah Khamenei amesema, uzalishaji wa athari katika tasnia ya usanii ikiwemo utengenezaji wa filamu za katuni una taathira katika kutambulisha fursa mbalimbali za bahari na akaongeza kwamba: kwa kutumia athari za kisanii na kutambulisha uwezo wa maendeleo ya bahari ya nchi, iwe ni katika sekta za kijeshi au sekta za ujenzi, kutazidisha shauku ya watu ya kutumia fursa hizo.
Katika mkutano huo, Adimeri Shahram Irani, kamanda wa Jeshi la Wanamaji, alitoa ripoti juu ya hatua na mipango inayotekelezwa na jeshi hilo katika sekta mbalimbali.

4103043

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha