IQNA

Wasomaji maarufu wa Qur'ani Tukufu / 16

Kwanini usomaji Qur'ani Tukufu wa Ustadh Abdul Basit una ushawishi na mvuto mkubwa?

19:47 - December 21, 2022
Habari ID: 3476280
TEHRAN (IQNA) - Baadhi ya maqarii au wasomaji Qur'ani Tukufu hulenga tu kuwa Lahni nzuri na Maqamat au mbinu za qiraa lakini katika upande wa pili usomaji wa Qur'ani Tukufu wa Ustadh Abdul Basit Abdul Samad ulikuwa rahisi lakini wakati huo huo wa kiroho, wenye ufanisi na kiufundi.

Wakati wa zaidi ya nusu karne ya shughuli zake kama qari au msomaji Qur'ani, Ustadh Abdul Basit Abdul Samad (Januari 1, 1927- Novemba 30, 1988) alisoma Qur'ani katika nchi nyingi na, kama alivyosema mwenyewe, usomaji wake ulisababisha mamia ya watu kuukubali Uislamu.

Kama qari mashuhuri, Abdul Basit alikuwa na sifa fulani. Kwa mfano aliweka thamani maalum kwa usomaji wa Qur'an na alikuwa na mazoea ya kusali Sunna kabla ya kila kisomo. Hatuu hii anasema ilimsadia kusoma Qur'ani Tukufu kwa hali maalum ya kiroho. Baadhi ya visomo vyake bora vilikuwa kabla ya sala ya alfajiri, ambayo inachukuliwa kuwa wakati mzuri zaidi wa kiroho na kutakabaliwa maombi au dua. Mahali pa usomaji au qiraa pia palikuwa muhimu. Kwa mfano alisoma Sura Al-Hashr na At-Takwir kwenye Msikiti wa Al-Kadhimiya au Haram ya Al Kadhimayn nchini Iraq na usomaji wake hapo unachukuliwa kuwa miongoni mwa bora zaidi.

Sauti ya Ustadh Abdul Basit ni ya kipekee na ndiyo maana mtu yeyote anayetaka kumwiga anajaribu kuifanya sauti yake isikike kama ya Abdul Basit. Mtindo wake unaweza kuelezewa kuwa ni Sahl na Mumtana, hiyo ni kusema kuwa ulikuwa ni mtindo rahisi. Usomaji wake hauna ugumu wa kisomo cha Mustafa Ismail, Kamil Yusuf Bahtimi, Mohamed Umran, Sheikh Rif’at, au wengineo. Abdul Basit alisoma moja kwa moja na zaidi bila ya kupanda na kushuka.

Nukta nyingine kuhusu kisomo chake ni kwamba alikuwa amejitolea kufuata kikamilifu kanuni za Qira’at na kuepuka kupindukia au kufurutu ada. Kama mtu anataka kuwa qari mzuri na kujenga msingi mzuri katika usomaji wa Qur'an, mfano bora zaidi kwake anaweza kuwa Ustadh Abdul Basit. Sauti ya mtu inaweza isiwe nzuri kama yake lakini anaweza kujifunza Lahn na mazingira ya usomaji kutoka kwa Ustadh Abdul Baist.

Halikadhalika Ustadh Abdul Basit ana mfululizo wa visomo vya Qur'ani Tukufu vilivyofanywa katika vikao maalumu vya Qur'ani Tukufu.

Katika kisomo chake, Ustadh Abdul Basit ana uwezo wa juu katika kuzingatia maana, imani na hadhi tukufu ya Qur'ani Tukufu. Hizi ni baadhi ya nukta ambazo huweza kubainisha umahiri wa msomaji Qur'ani Tukufu. Alitumia talanta na ujuzi wake wote kufikia kiwango cha juu zaidi cha usomaji mzuri unaomgusa msikilizaji.

Hapa chini ni klipu ya mojawapo ya visomo vyake vya kukumbukwa vya Sura za Qur'ani Tukufu za Al-Balad na Ash-Shams.

captcha