IQNA

Wasomaji Maarufu wa Qur'ani Tukufu /17

Abulainain Shuaisha; Msomaji Qur’ani mwenye lakabu ya Sheikh ul-Qurra

21:06 - December 24, 2022
Habari ID: 3476295
TEHRAN (IQNA) –Ustadh Abulainain Shuaisha alijulikana kama Sheikh ul-Qurra (kiongozi wa wasomaji Qur’ani) wa Misri. Alikuwa msomaji mashuhuri wa Qur’ani na mtu wa mwisho kutoka katika ‘kizazi cha dhahabu’ cha wasomaji Qur’ani wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Akiwa amezaliwa tarehe 22 Agosti 1922, Abulainain Shuaisha alitumia maisha yake katika kujaribu kufufua mitindo halisi ya qiraa au usomaji Qur’ani. Alielezewa kama mtu mashuhuri katika usomaji wa Qur'an na mmiliki wa 'sauti ya chuma'.

Alianza kusoma Qur'an Tukufu katika umri mdogo na mara akaingia kwenye duru za Qur'ani zilizohudhuriwa na wasomaji mashuhuri. Baadhi wamemchukulia kuwa msomaji ambaye itakwa vigumu kupatikana mfano wake katika uwanja wa usomaji wa Qur’ani Tukufu.

Ustadh Shuaisha alikuwa na sauti halisi ambayo ilielezewa kama "sauti ya chuma" kwa sababu ilikuwa na nguvu sana na kama chuma na ilisikika kwa ubora wa juu zaidi.

Wasoomaji wengi hujaribu kuiga mtindo wa qiraa ya Ustadh Shuaisha lakini hakuna anayeweza kufanya hivyo kikamilifu kwa sababu mtindo na sauti yake vilikuwa vya kipekee na vigumu sana kuiga.

Yeye, pamoja na Ustadh Abdul Basit Abdul Samad, alikuwa mwanzilishi mwenza wa Muungano wa Wasomaji Qur'ani wa Misri, na mwaka 1988, akawa rais wa umoja huo.

Ustadh Shuaisha alisafiri katika nchi nyingi kwa ajili ya kusoma Qur’ani na aliheshimiwa kwa usomaji wake mzuri huko Lebanon, Syria, Iraqi, Uturuki na Jordan, miongoni mwa zingine.

Alikuwa ni Qari wa kwanza wa Misri ambaye alisoma Qur’ani Tukufu katika Msikiti wa al-Aqsa katika mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem).

Ustaidh Shuaisha pia alisafiri hadi Iran mara kadhaa na aliwahi kuwa mjumbe wa jopo la majaji katika mashindano kadhaa ya kimataifa ya Qur'ani nchini humo.

Qari huyo mashuhuri alirejea kwa Mola wake Juni 23, 2011, akiwa na umri wa miaka 89 baada ya kuugua kwa muda wa miezi mitatu.

Hapa chini ni klipu ya usomaji wa Ustadh Shuaisha wa aya za Sura al-Infitar katika Msikiti wa Imam Hussein (AS) wa Cairo mnamo 1974.

captcha