IQNA

Qari Mashuhuri

Mwanae Abdul Basit anaangazia upendo wake kwa Qur'ani

17:50 - December 02, 2024
Habari ID: 3479842
IQNA - Mtoto wa qari mashuhuri wa Misri Abdul Basit Abdul Samad amesisitiza mapenzi ya baba yake kwa Qur'ani Tukufu.

Tariq Abdul Samad alizungumza katika mahojiano ya redio kuhusu baba yake katika kumbukumbu ya miaka 36 ya kifo chake.

Alisema Abdul Basit alikuwa mkarimu sana na alimtazama yeye na kaka yake kama marafiki.

Kuwa mtoto wa Abdul Basit ni baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo inaleta jukumu kubwa, alisema.

Tariq aliitaja Taqwa (kumcha Mungu), kuipenda Qur'ani na kuyafanyia kazi mafundisho yake ambayo yanatokana na mapenzi yake na heshima yake kwa Kitabu kitukufu kama urithi wa Abdul Basit.

"Shukrani kwa baraka za Qur'ani, watu bado wanatupenda, na kumbukumbu ya baba yangu iko hai kwani watu wanapenda kusikia sauti yake kila siku," aliongeza.

Abdul Basit Abdul Samad alikuwa qari mashuhuri ambaye alianzisha shule yake mwenyewe ya usomaji wa Kurani na kuwatia moyo wale wanaoipenda Quran duniani kote.

Alipewa jina la utani mara nyingi kama "Sauti kutoka Mbinguni," "Sauti ya Makka," na "Koo la Dhahabu."

Qiraa yake nzuri hata uliwavutia wasio Waislamu, ambapo mwanazuoni wa Kikristo aliwahi kuchagua sauti yake ya kipekee ya kusoma Qur'ani kama mada ya tasnifu yake ya Shahada ya Uzamivu.

Sheikh Abdul Basit Abdul Swamad alikuwa miongoni mwa maqarii na wasomaji mashuhuri wa kimataifa wa Qur'ani Tukufu na weledi wa masuala ya Qur'ani wanamtambua kuwa ndiye qarii mkubwa zaidi wa Qur'ami kote duniani. Ustadh Abdus Samad alibuni na kuanzisha mbinu makhsusi ya kiraa ya Qur'ani.

Abdul Basit alizaliwa mwaka 1927 katika kijiji cha Almazaizah katika eneo la Armant kusini mwa Misri. Babu yake, Ustadh Abdul Samad, alikuwa mtu aliyesifika kwa kuwa na takwa na kumcha Mwenyezi Mungu na miongoni mwa mahafidhi wa Qur'ani na vilevile mtaalamu wa masuala ya Qur'ani.

Sheikh Abdul Basit Abdul Swamad alikamilisha hifdhi ya Qur'ani akiwa na umri wa miaka 10 kijijini kwake kwa Ustadh Al Amir na akahitimu aina zote za kiraa ya Qur'ani akiwa na umri wa miaka 14.

Abdul Basit alipewa lakabu ya 'Koo ya Dhahabu' kutokana na kiraa yake ya kuvutia na alipendwa mno na wafuatiliaji wa masuala ya Qur'ani kwa kadiri kwamba hadi sasa anatambuliwa kuwa qarii mashuhuri na anayepesndwa zaidi wa Qur'ani.

Alianza kujifunza Qur'ani Tukufu akiwa bado mtoto mdogo na alipewa tuzo ya kuhifadhi na kusoma Qur'ani akiwa na umri wa miaka 12. Kipindi fulani Sheikh Abdul Basit alitumia muda wake mwingi kusafiri katika nchi za Kiislamu na kuwahamasisha watu kusoma kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Mwaka 1952 Sheikh Abdul Swamad alikwenda kuhiji Makka na kusoma Qur'ani katika Masjidul Haram na Masjidunnabi huko Madina. Vilevile alikwenda Palestina na kusoma Qur'ani huko Baitul Muqaddas na katika Haram ya Nabii Ibrahim AS

Qiraa ya Sheikh Abdul Basit Abdul Swamad iliwaathiri watu wengi na hata kuwavutia wasiokuwa Waislamu katika dini ya Kiislamu. Watu 6 waliingia katika dini ya Kiislamu baada ya kuathiriwa na kiraa yake mjini Los Angeles huko Marekani. Aidha inadokezwa kuwa nchini Uganda jumla ya watu 92 walisilimu katika majlisi ya kiraa ya msomaji huyo mashuhuri na watu wengine 72 pia walikubali dini tukufu ya Kiislamu katika majlisi nyingine baada ya kuvutiwa mno na usomaji wake.

Mwishoni mwa umri wake, Sheikh Abdul Basit alipatwa na maradhi ya kisukari na baadaye uvimbe wa ini. Alipelekwa London Uingereza kwa ajili ya matibabu baada ya kuzidiwa na maradhi na kurejeshwa Cairo wiki mbili baadaye. Inasemekana kwamba Sheikh Abdul Basit Abdus Samad alikuwa amehisi kwamba siku zake za kuishi duniani zinakaribia ukingoni na wakati wa kukutana na Mola Muumba ulikuwa unakaribia.

Qari huyo mashuhuri wa Misri aliaga dunia tarehe 30 Novemba mwaka 1988 katika mji mkuu wa Misri, Cairo. Maelfu ya maashiki wake walihudhuria mazishi yake. Mazishi hayo pia yalihudhuriwa pia na mabalozi wa nchi za Kiislamu mjini Cairo.

Sheikh Abdul Basit ameacha kanda nyingi za Sauti ya qiraa yake ya Qur'ani Tukufu ambazo bado zinawavutia wengi wengi duniani.

4251530

captcha