IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu / 49

Mafundisho ya Sura Al-Hujurat kuhusu kukabiliana na ubaguzi wa rangi

20:07 - December 21, 2022
Habari ID: 3476281
TEHRAN (IQNA) – Moja ya matatizo sugu katika dunia ya sasa ni ubaguzi wa rangi. Ingawa jitihada zimefanywa ili kukabiliana na jambo hilo baya, inaonekana kwamba kutozingatia mafundisho ya kidini kumezuia jamii kuondokana kabisa na ubaguzi wa rangi.

Al-Hujurat ni jina la sura ya 49 ya Qur'ani Tukufu. Sura hii ni Madani (imeteremshwa Madina) na iko katika juzuu ya 26. Ina aya 18 na ni Sura ya 107 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume (SAW).

Hujurat ni wingi wa neno Hujra kwa Kiarabu na maana yake ni vyumba. Ni neno lililotajwa katika aya ya 4 na linahusu vyumba vilivyojengwa kando ya Msikiti wa Mtume SAW huko Madina kwa ajili ya wake zake.

Sura Al-Hujurat inajumuisha kanuni za kimaadili kuhusu masuala kama vile uhusiano na Mwenyezi Mungu na Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) na jinsi watu wanapaswa kuingiliana wao kwa wao katika jamii. Vile vile inarejelea kigezo cha ubora wa baadhi ya watu juu ya wengine, haja ya kutawala utaratibu katika jamii, na ukweli wa imani na Uislamu.

Sura Al-Hujurat inawaamuru Waislamu kutozingatia uvumi, kuepuka kusengenya, kujuzuia kidukua makosa na wengine, na kujaribu kukuza maelewano kati ya Waislamu.

Aya za kwanza zinawataka waumini “wasiwe mbele mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake,” Enyi mlio amini! Msitangulie mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua."

Aidha aya ya pili ya sura hii inawafundisha jinsi ya kuzungumza na Mtukufu Mtume (SAW) kwa kusema: " Enyi mlio amini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii, wala msiseme naye kwa kelele kama mnavyo semezana nyinyi kwa nyinyi, visije vitendo vyenu vikaharibika, na hali hamtambui."

Sura pia inawaamrisha waumini kuwa makini na habari zinazoenezwa na waovu na waulize kwanza kabla ya kuwaamini.

Pendekezo jengine katika sura hii ya Qur'ani Tukufu ni kwamba iwapo kutatokea ugomvi baina ya baadhi ya makundi ya waumini, ni wajibu wa wengine kujitahidi kutafuta suluhu na kutengeneza njia ya utatuzi wa masuala hayo.

Sehemu nyingine ya Sura inarejelea sifa sita zisizofaa katika maingiliano ya kijamii, nazo ni kuwadhihaki wengine, kutafutana makosa, kukashifu wengine, kuwa na shaka juu ya mtu mwingine, kufanya ujasusi, na kusengenyana.

Katika Sura hii, imesisitizwa kwamba masuala kama vile rangi ya ngozi, rna kabila yasichukuliwe kuwa ni fahari kwa sababu kigezo cha utukufu na kuheshimiwa mbele ya Mwenyezi Mungu ni Taqwa (kumcha Mungu). Hayo yamo kwenye aya ya 13 ya Sura hii ifuatavyo: " Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari."

Aya za mwisho za Sura zinafafanua tofauti kati ya Uislamu na imani.

captcha