IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu /54

Muujiza wa Mtume Mtukufu SAW wa kupasuka kwa mwezi umetajwa katika Sura Al-Qamar

20:35 - January 07, 2023
Habari ID: 3476368
TEHRAN (IQNA) – Wanasayansi hawajapata sababu ya mpasuko unaoonekana katika mwezi lakini baadhi yao wanasema mpasuko huo ulijiri mamia ya miaka iliyopita.

Kwa mujibu wa Sura Al-Qamar ya Quran Tukufu, ni muujiza wa Mtukufu Mtume (SAW).

Al-Qamar ni sura ya 54 ya Qur'ani Tukufu ambayo ina aya 55 na iko katika Juzuu ya 27. Ni Makki (iliteremshwa katika mji wa Makka) na ni Sura ya 37 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Qamar, ambayo ina maana ya Mwezi, inakuja katika aya za kwanza na hivyo Sura imepewa jina hilo.

Ni ukumbusho wa muujiza wa Mtume Mtukufu (SAW) wa kupasuka kwa mwezi. Wakati Mushrikin (washirikina) wa Makka walipoomba muujiza kuthibitisha ukweli wake, Mtume (SAW) aligawanya mwezi kwa kuunyooshea kidole kisha akaurudisha pamoja. Muujiza huu unajulikana kama Shaq al-Qamar (kugawanyika kwa mwezi).

Mushrikin, hata hivyo, walikataa kuamini hata baada ya muujiza huu, wakimtuhumu mtukufu huyo kwa uchawi na uwongo.

Mwanajiolojia wa Misri Dk. Zaghloul Annajar katika kitabu kilichochapishwa mwaka 2004 amezungumzia suala la kupasuka kwa mwezi. Katika kitabu hiki, kuna picha ambayo imepelekea wanasayansi wa NASA kusema kuwa mwezi uliwahi kugawanyika  katika nusu mbili zamani na kuna uthibitisho wa hilo katika muonekano wa mwezi.

Aya za Surah Al-Qamar nyingi ni maonyo dhidi ya madhalimu. Zinaashiria juu ya watu ambao waliishi hapo awali na kufanya maovu. Aya zinatahadharisha kuwa watu hao watakuwa katika hali ngumu pale yatakapochunguzwa matendo yao Siku ya Kiyama.

Huu ni ukumbusho kwa watu kujifunza somo. Watu waliotajwa katika Sura hii ni watu wa Adi, Thamud, Lut na Firauni.

Sura inasisitiza kuwa Qur'ani Tukufu imefanywa kuwa rahisi ili kila mtu apate mafunzo kutoka kwayo. Hili limetajwa katika aya za 17, 22, 32 na 40 za Sura.

  "Tumeifanya Qur'an kuwa nyepesi kueleweka, lakini je, kuna yeyote anayezingatia?"

Sura hii inawaonya wale wanaofuata matamanio ya nafsi zao ingawa wamefahamishwa Siku ya Kiyama na yatakayowapata katika dunia hii na kesho Akhera.

Sura pia inasimulia hadithi za wale waliokadhibisha Mitume wa Mwenyezi Mungu na adhabu walizozipata.

captcha