IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu / 46

Hatima ya wanaomkanusha Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama kama ilivyoelezwa katika Surat Al-Ahqaf

20:55 - December 10, 2022
Habari ID: 3476225
TEHRAN (IQNA) – Watu wanaishi kwa uhuru wakiwa na imani na mawazo tofauti. Wanaweza kukataa ukweli na kufuata mawazo ya uwongo lakini wanapaswa kujua nini hatima inayowangoja wale wanaoikadhibisha ukweli na kufuata uwongo.

Al-Ahqaf ni jina la sura ya 46 ya Qur'ani Tukufu. Ni Sura ya Makki ambayo ina Aya 35 na iko katika Juzuu ya 26. Ni Sura ya 66 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Jina la sura hii linatokana na neno Ahqaf katika aya ya 21, ambayo ina kisa cha watu wa A’ad na Mtume Hud (AS) ambaye aliwaonya watu wa A’ad kuhusu adhabu ya Mwenyezi Mungu lakini walikataa kusikiliza. Ahqaf maana yake ni ardhi yenye mchanga na mahali walipokuwa wakiishi watu wa A’ad palikuwa na mchanga. Neno Ahqaf limetajwa katika Qur'ani Tukufu mara moja tu.

Sura Al-Ahqaf inahusu Siku ya Kiyama na hadhi ya waumini na makafiri siku hiyo. Inasema ulimwengu haujaumbwa bure. Inasisitiza  kwamba Mwenyezi Mungu anaweza kuwafufua wafu. Pia inatilia mkazo ulazima wa mtu kuwatendea vizuri wazazi.

Kwa mujibu wa baadhi ya Hadithi, aya ya 15 ya Sura hii inamhusu Imam Hussein (AS).

Imesemekana kwamba mtu yeyote anayesoma Surah Al-Ahqaf kila usiku au kila Alhamisi usiku, Mwenyezi Mungu ataondoa khofu moyoni mwake katika ulimwengu huu na ujao.

Makusudio ya Sura hii ni kuwaonya makafiri wanaokataa mwito wa kumwamini Mwenyezi Mungu, Mtume wake na Siku ya Kiyama. Inaonya juu ya adhabu kali kwa wanaokanusha. Sura inaanza kwa kuthibitisha Siku ya Kiyama na inakariri dhana hii katika aya zifuatazo.

Katika Sura hii, upweke wa Mungu na utume wa Muhammad (SAW) umesisitizwa. Pia inaashiria yale yaliyotokea kwa watu wa A’ad na vijiji vilivyo karibu na Makka, ikiwaonya makafiri wasirudie kosa lao.

Sura pia inasema baadhi ya majini walikuja kwa Mtukufu Mtume (SAW) na wakasilimu baada ya kusikia baadhi ya aya za Qur'ani Tukufu.

Wakati wa kuteremshwa kwa Sura hii, makafiri wa Makka walijiona kuwa wako kwenye kilele cha madaraka na walifikiri kwamba hawangehitaji kuukubali mwaliko wa Mtukufu Mtume (SAW). Ndio maana wakaendekeza ibada ya masanamu na kuwapotosha watu na wakawa wanakejeli na kukanusha ukweli wa Uislamu na Quran.

Surat Al-Ahqaf iliteremshwa kwa ajili ya kuwaonya makafiri wa Kabila la Quraysh huko Makka na kuwakumbusha yale yanayowangoja katika dunia na akhera ikiwa wataendelea na ukanushaji wao na kufuata njia ya uwongo.

Habari zinazohusiana
captcha