IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu /51

Madhumuni ya uumbaji katika Sura Adh-Dhariyat

17:38 - December 26, 2022
Habari ID: 3476311
TEHRAN (IQNA) – Viumbe vyote vimeumbwa na Mwenyezi Mungu na kila mmoja wao ana nafasi na lengo katika dunia. Wanadamu, kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu, ikiwa ni pamoja na Surah Adh-Dhariyat, wameumbwa kumwabudu Mungu ili wafikie hatima yao.

Adh-Dhariyat ni sura ya 51 ya Qur'ani Tukufu. Ina aya 60 na iko kwenye Juzuu za 26 na 27 za Qur'ani Tukufu. Ni Makki na ni Sura ya 67 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Neno Dhariyat, ambalo jina la Surah linatokana na hilo, limetajwa katika aya za kwanza na ni aina ya wingi ya Dhariya, ambayo ina maana ya upepo unaotawanya vitu angani.

Mada kuu ya Sura ni Siku ya Kiyama. Pia imezungumzia Tauhidi, Ishara za Mwenyezi Mungu duniani, Malaika wanaokwenda nyumbani kwa Ibrahim (AS) wakiwa wageni, adhabu kwa watu wa Lut (AS), na hadithi za Musa (AS), kaumu ya A'ad, watu wa Thamud na kaumu ya Nuhu (AS).

Surah Adh-Dhariyat inaanza kwa viapo vinne vya Mwenyezi Mungu ikisisitiza kwamba ahadi za Mwenyezi Mungu kuhusu Siku ya Kiyama ni za kweli. Mwenyezi Mungu anaapa juu ya Dhariyat, Hamilat, Jariyat, na Muqsimat na anasisitiza kwamba kile alichoahidi kitatimia.

Aya zifuatazo zinakosoa fikira dhaifu za wale wanaokanusha ufufuo na kuwaonya kwamba adhabu inawangoja. Kisha Sura inaeleza sifa za wachamungu, ikisema wanaswali usiku na kutoa sadaka.

Vile vile inabainisha baadhi ya ishara za Mwenyezi Mungu katika ardhi na kusema kwamba mbingu ndio chanzo cha Riziki kwa watu.

Sura inasimulia hadithi za baadhi ya Mitume, akiwemo Ibrahim, Musa, Lut, Saleh na Nuhu-amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yao.

Sehemu ya mwisho ya Sura tena inasisitiza dalili za uwezo wa Mwenyezi Mungu, ikasisitiza kwamba watu watarejea kwa Mwenyezi Mungu, na inakataa aina yoyote ya Shirki.

Vile vile inawakosoa wale wanaokataa mwaliko wa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) kwa Mwenyezi Mungu, na kuwakumbusha yale yaliyotokea kwa watu walioishi kabla na wakafanya hivyo hivyo na kuwaonya kuhusu Siku ya Hukumu.

Jambo muhimu katika Sura hii ni kwamba inawaweka wanadamu na majini pamoja na kusema Mwenyezi Mungu alikuwa na lengo moja la kuumbwa kwao.

Katika aya ya 56 ya Sura Mwenyezi Mungu SWT anasema: “Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi."

Kwa mujibu wa Tafsiri ya Qur'ani Tukufu ya Al-Mizan, aya hii inaonyesha kwamba kumwabudu Mwenyezi Mungu ndilo lengo kuu la kuumbwa kwa wanadamu na kwamba kunavutia msamaha na rehema za Mwenyezi Mungu.

captcha