IQNA

Sura za Qur’ani Tukufu / 50

Majibu kwa wakanushaji katika Sura Qaaf

21:42 - December 24, 2022
Habari ID: 3476296
TEHRAN (IQNA) – Ufufuo na maisha baada ya kifo ni masuala ambayo yamesisitizwa katika mafundisho ya Kiislamu. Sura Qaaf ni moja ya sura za Qur'ani Tukufu ambayo inajibu maswali yaliyoulizwa na wale wanaofikiria maisha kuwa ni ya ulimwengu huu na wanaikana akhera.

Qaaf ni jina la sura ya 50 ya Qur’ani Tukufu, ambayo ina aya 45 na iko katika Juzuu  ya 26. Qaaf ni Makki,  yaani iliteremshwa katika mji mtakatifu wa Makka, na ni Sura ya 34 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Inaanza na herufi Qaaf (herufi ya Kiarabu) na hivyo basi jina la Sura linatokana na herufi hiyo.

Ufufuo, mshangao wa makafiri wanapoona kurejea kwenye uhai waliofariki, Utume, Tauhidi, na uwezo wa Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa katika sura hii.

Inaelekeza kwenye wito wa Uislamu na kile kinachojumuisha dini hii tukufu, kama vile ufufuo.  Sura  hii imetoa majibu kwa maswali yaliyoulizwa na wakanushaji na inawaonya kwamba wakikataa kushika njia ya uwongofu itawapelekea kuangamia.

Sura hii aidha  inathibitisha uwezo na elimu ya Mwenyezi Mungu isiyo na kikomo kwa kutaja mifano kama vile uumbaji wa mbingu na ardhi, pambo la mbingu kwa nyota, upanuzi wa ardhi na uumbaji wa milima, ukuaji wa mimea, kutuma maji kutoka mbinguni na kuhuisha ardhi kwa hayo.

Kisha inamrejelea mwanadamu, ikibainisha kwamba maisha yake na matendo yake yameandikwa kwa usahihi tangu siku aliyozaliwa hadi atakapokufa na kueleza yatakayompata baada ya kufufuliwa. Sura inabainisha kuwa Siku ya Kiyama hupimwa amali zake zote na kwa kuzingatia hilo, ima atakuwa miongoni mwa wafanyao wema na kwenda peponi au atakuwa miongoni mwa madhalimu na kwenda kwenye moto wa Jahannamu.

captcha