IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Lengo la maadui ni kubadilisha utambulisho wa taifa la Iran na Mapinduzi ya Kiislamu

6:58 - March 22, 2023
Habari ID: 3476740
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema maadui wanapinga Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini (MA), na maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu kila mwaka, sambamba na kuupinga mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini Iran; na kusisitiza kuwa, lengo la maadui ni kubadilisha utambulisho wa taifa hili na Mapinduzi ya Kiislamu, na badala yake walete demokrasia bandia ya Kimagharibi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo Jumanne katika hotuba yake kwa mnasaba wa Nowruz, yaani siku ya kwanza ya mwaka mpya wa 1402 Hijria Shamsia aliyoitoa katika Haram ya Imam Ridha (AS) katika mji mtakatifu wa Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran na kueleza kuwa, "Sisi tunazungumza kuhusu mageuzi na ustawi, na maadui pia wanazungumza kuhusu mabadiliko, lakini tunachomaanisha na wanachomaanisha ni tofauti, wao wanataka kubadilisha utambilisho wetu."

Ayatullah Ali Khamenei amebainisha kuwa, Ustikbari na Uzayuni ni maadui wa Iran ya Kiislamu, na wanapiga vita utambulisho wa Jamhuri ya Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu ameeleza bayana kuwa, lengo la maadui ni kuhujumu kila kitu ambacho kinawakumbusha wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu Mapinduzi (ya Kiislamu) na Uislamu.

Amefafanua kwa kusema: Maadui wanapinga kukaririwa jina la Imam (Khomeini), Faqih Mtawala, Siku ya Quds, na uchaguzi. Wanapozungumza kuhusu mabadiliko, wanalenga kubadilisha utambulisho, utamaduni na mfumo wa Kiislamu hapa nchini.

Kadhalika amewakosoa wanaoeneza sumu ya kudai Katiba mpya hapa nchini na kueleza bayana kuwa, inasikitisha kuona baadhi ya Wairani wameingiwa na kasumba hiyo ya kudai Katiba, ama kwa malengo maalumu au bila kuwa na ufahamu wa lengo halisi la maadui la kutaka kubadilisha mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini.

Kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemshukuru Allah kwa kumjaalia aweze kutoa hotuba mbele ya ummati baada ya kusimamishwa kwa miaka kadhaa kutokana na janga la Corona. Katika kipindi cha Corona, Ayatullah Sayyid Khamenei alitoa hotuba hiyo kwa njia ya video.

Amewashukuru madaktari na wahudumu wa afya wa Iran kwa jitihada zao za kukabiliana na tandavu ya ugonjwa wa COVID-19, huku akimuomba Allah kuliondoa janga hilo duniani kikamilifu. 

Hapo awali katika ujumbe wake wa Nowruz, Ayatullah Khamenei alitaja uchumi na maisha ya wananchi kuwa ndilo lililokuwa suala muhimu zaidi la nchi mwaka jana, na kusisitiza kuwa uchumi ndio suala kuu la nchi mwaka huu pia; amesema: Kaulimbiu ya 1402 ni 'Udhibiti wa Mfumuko wa Bei, Ukuaji wa Uzalishaji'.

4129347

captcha