IQNA

Ujumbe wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa munasaba wa Nowruz

1402; Mwaka wa 'Udhibiti wa Mfumuko wa Bei, Ukuaji wa Uzalishaji

11:22 - March 21, 2023
Habari ID: 3476735
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, ametuma ujumbe kwa mnasaba wa Nowruz (Nairuzi) ambayo ni siku kuanza mwaka mpya wa 1402 Hijria Shamsia ambapo ametoa pongezi kwa wananchi wa Iran na mataifa yote yanayosherehekea Nowruz.

Katika ujumbe huo Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametaja uchumi na maisha ya wananchi kuwa ndilo lililokuwa suala muhimu zaidi la nchi mwaka jana, na kusisitiza kuwa uchumi ndio suala kuu la nchi mwaka huu pia; amesema: Kaulimbiu ya 1402 ni 'Udhibiti wa Mfumuko wa Bei, Ukuaji wa Uzalishaji'.

Mwanzoni mwa ujumbe wake wa Nowruz, Ayatullah Khamenei amezungumzia kuambatana kwa msimu wa machipuo ya maumbile na msimu wa machipuo ya kiroho (mwezi wa Ramadhani) na kusema: Upepo mwanana wa hali ya kiroho katika mwezi mtukufu wa Ramadhani unajumuisha watu wote na kwa msingi huo tunapaswa kuziweka nyoyo zetu mbele upepo huo wa Mwenyezi Mungu na kuzipamba kwa harufu nzuri ya upepo huo. 

4129264

Ayatullah Khamenei ameashiria kwa ufupi matukio ya mwaka uliomalizika jana wa 1401 na kusema, mwaka huo, kama ilivyokuwa miaka yote ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, umeandamana na mambo mbalimbali matamu na machungu. Amesisitiza kuwa uchumi ulikuwa suala muhimu zaidi la nchi katika mwaka uliopita na kuongeza kuwa: Kwa upande wa uchumi, kulikuwa na machungu na matamu; machungu yalihusiana zaidi na mfumuko wa bei na bei za juu, hasa bei za juu za vyakula na mahitaji ya msingi ya maisha, ambazo zimeongezeka sana, na shinikizo kubwa lilikuwa juu tabala la wanyonge katika jamii.

Amesema: Bila shaka, kazi nzuri na ustawi zimefanyika katika sekta ya uchumi, na zinapaswa kuhusishwa na maisha ya watu. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja himaya iliyotolewa kwa sekta ya uzalishaji mwaka 1401 kwa kuanzishwa upya maelfu kadhaa ya viwanda vilivyokuwa vimesimama, ongezeko la makampuni ya kisayansi na kielimu na kupungua asilimia ndogo ya ukosefu wa ajira nchini kuwa ni miongoni mwa hatua chanya zilizochukuliwa katika sekta ya uchumi. Amesema: Nukta nyingine ya kufurahisha ya sekta ya uchumi mwaka jana ilikuwa maonyesho ya uwezo na mafanikio ya wazalishaji wa serikali na wasio wa serikali na kukutana na wazalishaji wakuu wa nchi katika Huseiniya ya Imam Khomeini (MA).

Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba uamuzi wake kuhusu hatua za wazalishaji nchini ni chanya na kuongeza kuwa: "Nasema kwa msisitizo kwamba, kazi nzuri zinazofanywa katika sekta ya uchumi zinapaswa kuishia kwenye kufunguka kwa maisha ya wananchi hasa tabaka la wanyonge, na suala hili haliwezekani isipokuwa kwa mipango makini na mwendelezo wa kazi hizi."

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, matatizo ya kiuchumi si ya Iran pekee bali takriban nchi zote zikiwemo nchi zenye uchumi imara na zilizoendelea pia zinakabiliwa na matatizo ya kiuchumi na hata kufilisika kwa benki na madeni makubwa. Amesema: Viongozi wa serikali pamoja na wanaharakati wa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni wanapaswa kufanya kila wawezalo ili kuufanya mwaka huu kuwa mwaka mtamu kwa taifa la Iran kwa kupunguza machungu na kuongeza mafanikio.

Kuhusu mwaka mpya wa 1402 Hijria Shamsia, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Suala kuu na la msingi la nchi mwaka huu pia ni uchumi. Hii haina maana kwamba hakuna matatizo katika sekta nyingine. Kuna matatizo mbalimbali ya kiutamaduni na kisiasa nchini, lakini ikiwa Serikali, Bunge, wanaharakati wa uchumi na makundi ya wananchi vijana na wenye ari yataweka juhudi zao zote katika kutatua matatizo ya watu, matatizo mengine mengi pia yatatatuliwa.

Ameongeza kuwa: Kwa kuzingatia vipengele vyote hivyo, hasa suala la mfumuko wa bei ambalo ni tatizo kuu, na pia uzalishaji ambao ni miongoni mwa funguo muhimu za kuinusuru nchi na matatizo ya kiuchumi, natangaza kaulimbiu ya 1402 kuwa ni 'Udhibiti wa Mfumuko wa Bei, Ukuaji wa Uzalishaji'.

captcha