IQNA

Jinai za Israel

Nchi za Kiislamu zalaani hujuma ya Wazayuni dhidi ya Msikiti wa al Aqsa

16:30 - May 19, 2023
Habari ID: 3477016
TEHRAN (IQNA)- Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na nchi za Kiislamu zimelaani hujuma iliyofanywa na Wazayuni wakiongozwa na mawaziri na wabunge kadhaa wa utawala haramu wa Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa katika kile kilichopewa jina la "siku ya bendera".

Katika taarifa yake, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu sambamba na kulaani hujuma ya maafisa wa utawala wa Kizayuni na walowezi dhidi ya Msikiti wa al Aqsa, imeitaja hatua hiyo kuwa ni muendelezo wa sera za utawala wa Tel Aviv za  kuvunjia heshima maeneo matakatifu, uhuru wa kuabudu na ukiukaji wa wazi wa maazimio ya kimataifa.

Taarifa ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imeongeza kuwa, mji wa Quds ni sehemu muhimu ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu katika mipaka ya mwaka 1967, na mji mkuu wa Mnchi ya Palestina; na maamuzi na hatua zote zinazochukuliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa ajili ya kuuyahudisha mji huo zinakiuka na kupingana na maazimio ya kimataifa.

Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki pia imelaani vikali mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa chini ya ulinzi wa polisi ya Kizayuni.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imeitaka Israel kuepuka vitendo vya uchochezi na imetoa wito wa kuckuliwa hatua muhimu na kwa uzito mkubwa.

Kwa upande wake, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Misri pia imesema kwamba inalaani vikali hujuma iliyofanywa na maafisa wa serikali, wabunge wa utawala wa Israel na walowezi wa Kizayuni katika Msikiti wa Al-Aqsa katika fremu ya kile kinachoitwa "maandamano ya bendera" ambayo imeandamana na vitendo vya uchochezi kwa lengo la kuwabana Waislamu wanaotekeleza ibada ya Swala na kuchochea hisia za taifa la Palestina.

4141757

captcha