Taarifa zinasema mazungumzo yamefanyika ndani ya wizara ya vita ya Israel yakihusisha shirika la ujasusi la Shin Bet, polisi, idara ya magereza, na jeshi ili kuainisha hatua za ukandamizaji katika eneo hilo takatifu la Waislamu..
Vikwazo vilivyopendekezwa vitapunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya waumini watakaoruhusiwa kuingia msikitini, mahali ambapo kwa kawaida hushuhudia mikusanyiko mikubwa ya waumini wakati wa Ramadhani.
Chini ya mpango huo, ni idadi ndogo tu ya watu watakaoruhusiwa kuingia kwa wakati mmoja. Aidha, ni wanaume walio na umri wa zaidi ya miaka 55, wanawake walio na umri wa zaidi ya miaka 50, na watoto walio chini ya miaka 12 ndio watakaoruhusiwa kuingia katika Msikiti wa Al Aqsa, eneo la tatu kwa utakatifu katika Uislamu.
Kwa swala za Ijumaa za pamoja, mpango uliopendekezwa utaruhusu hadi waumini 10,000 tu.
Msikiti wa Al-Aqsa umekuwa kitovu cha mvutano katika miaka ya nyuma, hasa wakati wa Ramadhani. Eneo hilo, ambalo pia lina umuhimu wa kidini kwa Wayahudi na Wakristo, limekuwa uwanja wa makabiliano kadhaa kati ya vikosi vya usalama vya utawala katili wa Israel na waumini wa Kiislamu.
Mnamo Mei 2021, vikosi vya Israel vilivamia msikiti huo wakati wa Ramadhani, na kuwajeruhi mamia ya waumini. Ghasia hizo zilichochea mzozo wa siku 11 kati ya Israel na Hamas, uliopelekea vifo vya zaidi ya Wapalestina 250.
Matukio kama hayo yalitokea pia mwaka wa 2022, ambapo vikosi vya Israel vilifanya uvamizi mara kadhaa msikitini, wakiwaondoa waumini ili kuruhusu wageni wa Kiyahudi kuadhimisha Pasaka ya Kiyahudi (Passover).
Mwaka 2023, kabla ya vita vya Gaza kuanza, mapigano yaliongezeka katika eneo hilo, yakizua shutuma kutoka kwa jumuiya ya kimataifa. Wakati wa moja ya uvamizi huo, inaripotiwa kuwa vikosi vya usalama vya Israel viliharibu mali ya msikiti, kuwajeruhi makumi ya Wapalestina, na kuwakamata angalau watu 400.
Tangu Oktoba 7, 2023, utawala katili wa Israel umekuwa ukizuia waumini kuingia katika msikiti huo. Kabla ya swala za Eid al-Adha mwaka jana, vikosi vya Israel viliripotiwa kufunga njia ya kuingia msikitini, huku maafisa wa polisi wakiwazuia kwa nguvu vijana kufikia msikiti kwa kutumia marungu na nguvu za kimwili.
Wapalestina wengi wanachukulia ulinzi wa Msikiti wa Al-Aqsa kama jukumu la kitaifa, huku hatua kali za ukandamizaji za Israel katika eneo hilo zikionekana kama jaribio la kudhibiti kikamilifu msikiti huo na mazingira yake.
3492025