IQNA

Mahakama ya Bahrain yaidhinisha hukumu ya kifo dhidi ya wanaharakati

16:16 - June 17, 2020
Habari ID: 3472872
TEHRAN (IQNA)- Mahakama ya juu ya Bahrain hivi karibuni imeudhinisha hukumu ya kunyongwa vijana wawili wa nchi hiyo kwa kutegemea ushahidi bandia.

Malalamiko na maandamano ya wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala dhalimu wa nchi hiyo yalianza tarehe 14 Februri mwaka 2011. Mwanzoni walikuwa wakitaka kufanyika mabadiliko katika mfumo wa utawala wa nchi hiyo hasa kuondolewa ubaguzi, lakini taratibu maandamano hayo yalichukua sura mpya ya ghasia kufuatia hatua ya utawala wa Saudia ya kutuma askari wake katika nchi hiyo jirani kwa ajili ya kuwakandamiza wapinzani wa utawala wa Aal Khalifa. Utawala huo umekuwa ukitumia mbinu tofauti za kidikteta na za mkono wa chuma dhidi ya wapinzani ikiwa ni pamoja na kutolewa hukumu za kifo dhidi yao.

Tokea mwaka 2011 hadi sasa utawala wa Aal Khalifa umetoa hukumu bandia 40 za kifo dhidi ya watu wanaolalamikia uongozi mbovu wa watawala ambao ni vibaraka wa Saudia na nchi za Magharibi. Mahakama ya Juu ya Bahrain imekuwa ikiwaelekezea wapinzani wa utawala huo tuhuma bandia kama vile kushambulia askari usalama au kupanga njama za kutekeleza operesheni za kigaidi na hatimaye kuwapa vifungo vya muda mrefu na kutoa hukumu za kifo dhidi yao. Hukumu mbili zilizotolewa hivi karibuni dhidi ya vijana wawili wa nchi hiyo kwa kwa madai bandia kuwa waliwashambulia askari usalama pia zimetolewa kwa msingi huo huo. Hii ni katika hali ambayo vijana hao hawakuwa na kosa jingine ghairi ya kuukosoa utawala wa Manama kwa kuwakandamiza raia na kutozingatia matakwa yao.

Nukta nyingine ni kwamba utawala huo unawatesa wapinzani wake wa kisiasa na kuwalazimisha kukiri makosa wasiyohusika nayo kwa kutegemea tuhuma zisizo na msingi wowote. Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch na Kituo cha Haki za Binadamu na Demokrasia cha Bahrain yalitangaza siku chache zilizopita kwamba watu waliohukumiwa kifo wanasisitiza kwamba waliteswa na askari usalama na kulazimishwa kukiri makosa ambayo hawakuyafanya.

Tunaweza kusema kuwa uadilifu ambao unapaswa kuwa muhimili muhimu zaidi katika chombo na mfumo wa mahakama ya nchi yoyote ile, ni jambo lisiloonekana kabisa katika mahakama za Bahrain. Tuhuma bandia, kutolewa hukumu za kidhalimu na hasa kunyongowa na watuhumiwa kuteswa na kulazimishwa kukiri makosa wasiyohusika nayo ni vielelezo vya wazi vinavyoashiria kwamba mfumo wa mahakama wa Bahrain sio huru na wala hauwezi kutegemewa katika kutoa hukumu za kiuadilifu.

3471730

Kishikizo: bahrain aal khalifa
captcha