IQNA

Ugaidi

Hujuma msikitini Afghanistan yaua watu 11

18:24 - June 09, 2023
Habari ID: 3477122
Watu wasiopungua 11 waliuawa na makumi ya wengine walijeruhiwa baada ya kutokea shambulio la kigaidi katika msikiti mmoja mkoani Badakhshan, kaskazini mashariki mwa Afghanistan.

Shambulio hilo lililenga watu waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya kumuenzi na kumkumbuka afisa wa Taliban aliyeua katika shambulizi jingine Jumanne iliyopita. Hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulio hilo dhidi ya Msikiti waAbdul Nafi Takor.

Moazuddin Ahmadi, afisa wa Taliban anayehusika na habari na utamaduni, alisema Safiullah Samim, mkuu wa zamani wa polisi wa Taliban huko Baghlan ni miongoni mwa waliouawa.

Nissar Ahmad Ahmadi, Naibu Gavana wa mkoa wa Badakhshan aliuawa katika shambulio la bomu dhidi ya gari lililokuwa limembeba mkoani hapo. Kundi la ISIS lilikiri kutekeleza hujuma hiyo ya Alhamisi.

Wakati huo huo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani shambulio la kigaidi lililotokea jana huko Afghanistan na kuua na kujeruhi makumi ya watu.

Nasser Kan'ani amesema, Tehran inalaani kitendo chochote cha kigaidi ambacho kinahatarisha usalama wa nchi na wananchi wa Afghanistan.

Kadhalika amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa pole kwa serikali, kwa wananchi wa Afghanistan na familia za wahanga wa shambulio hilo lililolenga waumini waliokuwa msikitini huko kaskazini mashariki mwa nchi.

Aidha Kan'ani amewaombea dua na maghfira ya Mwenyezi Mungu wote waliouawa kwenye shambulio hilo la kigaidi, kama ambavyo amewaombea pia afueni ya haraka majeruhi.

3483864

captcha