IQNA

Watetezi wa Qur'ani

Iran na Jordan zalaani kukaririwa vitendo vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu Uswidi

20:27 - October 01, 2023
Habari ID: 3477679
TEHRAN (IQNA)- Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema: Serikali ya Uswidi inatakiwa kujibu matakwa ya wazi kabisa ya Waislamu kwa kuwajibika na kufuata kikamilifu kanuni za kimsingi za haki za binadamu, kwa kuhimiza maadili na kuishi pamoja kwa amani wafuasi wa dini tofauti na kuchukua hatua za kivitendo na zenye ufanisi.

Nasser Kan'ani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ambaye alikuwa akizungumzia vitendo vya kuvunjiwa heshima tena Qur'ani Tukufu nchini Uswidi ameongeza kuwa: "Inasikitisha kwamba, uvitendo vya kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu vinakaririwa kwa kukanyaga kanuni za msingi za haki za binadamu."

Kan'ani amesema: Vitendo vya chuki, matusi na mashambulizi dhidi ya haki na matukufu ya Waislamu zaidi ya bilioni mbili vimefanywa mbele ya polisi wa Uswidi ambao jukumu lao kuu ni kulinda usalama na kuzuia ukiukwaji wa haki za wengine; na hapana shaka kuwa vitendo hivyo kamwe havitasahauliwa na watu wenye mawazo huru na wanaotafuta ukweli duniani.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amefafanua kuwa: Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, madai ya maafisa wa serikali ya Uswidi kwamba wanapinga vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu, bila ya kuchukuliwa hatua, hayatoshi.

Kufuatia kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Uswidi, kulikofanywa mara kadhaa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliamua kutompokea balozi mpya wa Uswidi mjini Tehran; na balozi mpya wa Iran ambaye alitakiwa kwenda Stockholm, amezuiliwa kufanya hivyo hadi pale serikali ya Uswidi itakapobadilisha mienendo yake katika suala hili.

Awali Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Amir Abdollahian aliyefanya mazungumzo na mwenzake wa Uswidi huko mjini New York kandokando na mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, aliashiria vitendo vya kujeruhi hisia za Waislamu bilioni 2 duniani kwa vitendo vya mara kwa mara vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukuifu nchini Uswidi na kusema: "Ni jambo lisilokubalika kupuuza matukufu ya Waislamu bilioni 2 duniani kwa kisingizio cha kulinda maadili ya Uswidi."

Pia katika taarifa yake siku ya Jumamosi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jordan ililaani kuruhusu mtu huyo kunajisi nakala za Qur'ani Tukufu.

Wizara ilisema Jordan inapinga kukiuka utakatifu wa alama za kidini, ambayo inasababisha kuchochea chuki na vurugu na kutishia kuishi pamoja kwa amani.

Ilibainisha "haja" ya kukomesha na kuharamisha vitendo vya chuki, ikihimiza kuendelezwa kwa amani na uvumilivu, kukataa misimamo mikali na kutovumiliana na kukabiliana na chuki inayoongezeka ya Uislamu.

3485383

 

captcha