IQNA

Kimbunga cha Al Aqsa

Ayatullah Khamenei: Tukio la Kihistoria la Kimbunga cha Al Aqsa limevuruga sera za Marekani

16:10 - November 29, 2023
Habari ID: 3477965
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema tukio la kihistoria la Kimbunga cha al-Aqsa cha harakati ya Hamas kimsingi lilikuwa dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini limeweza kuvuruga sera za Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia na litaifuta kabisa ajenda hiyo.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo Jumatano katika hadhara ya mamia ya wanachama wa vikosi vya kujitolea vya Basij vya Iran mjini Tehran kwa mnasaba wa Wiki ya Kitaifa ya Basij. 

"Tukio la kihistoria la Kimbunga cha al-Aqsa lilikuwa dhidi ya utawala wa Kizayuni lakini pia limeweza kuvuruga jedwali la sera za Wamarekani katika eneo la Asia Magharibi, na Mungu akipenda, dhoruba hii ikiendelea, itasomba kabisa meza nzima ya ajenda hizo," amesema Kiongozi Muadhamu.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, ukatili wa Israel huko Gaza si tu kwamba unaufedhehesha utawala huo pekee bali pia Marekani, baadhi ya nchi za Ulaya na utamaduni na ustaarabu wa Magharibi.

Amesema: Vitendo vya kinyama na vya kikatili ambavyo utawala wa Kizayuni umefanya katika jinai zake dhidi ya watu wa Gaza, si tu kwamba vimeharibu sifa ya utawala huo pekee, bali pia Marekani. Ukatili huo umeharibu sifa ya nchi kadhaa mashuhuri za Ulaya, na sifa ya utamaduni na ustaarabu wa Magharibi.

Ameongeza kuwa: "Utamaduni na ustaarabu wa nchi za Magharibi ndio uleule ustaarabu ambao wakati watoto 5,000 wanapouawa kwa mabomu ya fosforasi, utawala wa nchi fulani ya Magharibi unasema Israel inajilinda. Je, huku ni kujilinda? Huu ndio utamaduni wa Magharibi, ambao umedharaulika.” 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ukatili wa Israel huko Gaza katika kipindi cha siku 50 zilizopita ni mukhtasari wa jinai za miongo kadhaa za utawala huo dhidi ya Wapalestina.

Ayatullah Khamenei amesema maafa ya siku 50 zilizopita ni sehemu ndogo ya jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Palestina zinazoendelea kwa muda wa miaka 75.

"Kimbunga cha Al-Aqsa hakitaisha, na wanapaswa kujua kwamba hali ya sasa haitaendelea."

Kiongozi Muadhamu pia amesisitiza kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu inaamini suala la kuitishwa kura ya maoni huko Palestina kwa kuzingatia maoni ya wananchi wa Palestina. Jamhuri ya Kiislamu haina mtazamo wa kuwatupa Wazayuni na Wayahudi baharini."

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei amesema Marekani imeshindwa katika njama zake za kuunda "Mashariki Mpya ya Kati," na kuongeza kuwa kile kinachoitwa "suluhisho la serikali mbili" katika ardhi za Palestina ni sehemu ya sera hiyo hiyo ya uhasama ambayo imeshindwa na kufeli vibaya.

4184755

Habari zinazohusiana
captcha