IQNA

Mawaidha

Hoja za Mantiki kuhusu ufufuo

16:03 - November 06, 2024
Habari ID: 3479708
IQNA - Kuna hoja nyingi za kimantiki zinazotolewa kama ushahidi wa ulazima wa kuwepo siku ya ufufuo au Kiyama.

Wanafalsafa wa Kiislamu na wanazuoni bingwa (Hakim) wameangazia baadhi ya nukta hizo  kurejelea Quran Tukufu.
Chini hapa ni baadhi ya hoja hizo:
A) Hoja ya Hikmat (hekima)
Ikiwa tunaamini kwamba hakutakuwa na ulimwengu mwingine baada ya huu, basi maisha yatakuwa tupu na yasiyo na maana. Kwa nini mtu aishi katika ulimwengu huu kwa miaka 70 au 80 au zaidi au chini ya hapo na kupitia taabu na majanga mbalimbali bila kutarajia kupata chochote kutoka humo?
Quran Tukufu inasema: “Je! Mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa? (Aya ya 115 ya Surah Al-Muminoun)
Inamaanisha kwamba ikiwa hakuna kurudi kwa Mungu, maisha hayangekuwa na maana yoyote. Maisha katika ulimwengu huu yanaweza kuwa na maana na kulingana na hekima ya kimungu ikiwa tu tutauona ulimwengu huu kama shamba na njia ya kuelekea ulimwengu unaofuata.
B) Hoja ya Haki.
Mungu amempa mwanadamu uhuru wa kuchagua na hiari ili kumjaribu na kumruhusu kukanyaga njia ya ukamilifu. Lakini vipi ikiwa mwanadamu atatumia vibaya uhuru huu? Vipi ikiwa wakandamizaji, wakosaji, na wapotovu wanatumia vibaya uhuru huo? Ni kweli kwamba baadhi ya watenda maovu wanaadhibiwa katika ulimwengu huu kwa yale waliyoyafanya, lakini si wote wanaadhibiwa kikamilifu kwa yote waliyofanya. Wala watu wema hawapati malipo yanayostahiki kwa matendo yao mema hapa duniani. Je! hiyo ni haki? Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 35-36 ya Sura Al-Qalam, “Je Kwani tutawafanya Waislamu kama wakosefu? Mna nini? Mnahukumu vipi?
Mtu anapaswa kutambua kwamba ili kutimiza haki ya Mwenyezi Mungu, ni muhimu kuwa na mahakama ya kimungu ambapo kila tendo dogo au kubwa linatathminiwa na kuainishiwa thawabu au adhabu. Vinginevyo, haki haitatimizwa. Hivyo basi, kuamini uadilifu wa Mwenyezi Mungu kunahitaji kuamini Ufufuo. Qur’ani Tukufu inasema katika Aya ya 47 ya Surah Al-Anbiya: “Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hisabu .”
C) Hoja ya Kusudi.
Kinyume na wanavyoamini wanamaada, katika itikadi ya Mwenyezi Mungu kuna lengo la kumuumba mwanadamu. Kwa maneno ya kifalsafa, lengo hili linaitwa ukamilifu, na katika Qur'ani na Hadithi ni ukaribu na Mungu au ibada ya Mungu.
Qur'ani Tukufu inasema katika Aya ya 56: “Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi".
Je, kusudi hili lingetimizwa ikiwa hakungekuwa na maisha baada ya kifo? Bila shaka, jibu ni hapana. Kuwe na ulimwengu mwingine baada ya huu ili njia ya ukamilifu ya mwanadamu iweze kuendelea na aweze kuvuna matunda ya kile alichokipanda katika ulimwengu huu.
Kwa hiyo, utimilifu wa lengo la uumbaji haungewezekana bila ya kuamini Ufufuo, na ikiwa tutakata uhusiano kati ya ulimwengu huu na ujao, kila kitu kitakuwa siri na hatutakuwa na majibu ya maswali kuhusu maisha.

3490572

Kishikizo: qiyama MAWAIDHA
captcha