IQNA

Hali ya Syria

Wakristo wa Syria wana wasiwasi kuhusu hatima yao chini ya utawala wa HTS

21:49 - December 28, 2024
Habari ID: 3479965
 IQNA – Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 13 nchini Syria, Wakristo walibaki waaminifu kwa serikali ya Bashar al-Assad. Lakini kunyakua madaraka kwa kasi kwa kundi la Hay’at Tahrir al-Sham (HTS) kumeongeza wasiwasi kuhusu hatima ya Wakristo walio wachache \ nchini humo.

Je, jamii ya Kikristo inayopungua nchini Syria inaweza kuendelea kuwepo chini ya utawala mpya wa HTS? Na je, Wakristo wa Syria waliobaki waaminifu kwa serikali ya Assad wanaweza kuamini ahadi za watawala wapya nchini humo? Kuna  maswali mengi kuhusu mustakabali wa Wakristo nchini Syria, ambayo yanajadiliwa katika Makala hii.

Kulingana na ripoti ya shirika lisilo la kiserikali la Kikristo lenye makao yake Marekani, idadi ya Wakristo nchini Syria kabla ya kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2011 ilikuwa milioni 1.5, yaani takriban asilimia 10 ya idadi ya watu nchini humo. Hata hivyo, ndani ya muongo mmoja, idadi yao ilipungua sana, na kufikia mwaka 2022, ni Wakristo 300,000 tu waliosalia nchini humo, yaani takriban asilimia 2 ya idadi ya watu wa Syria. Ingawa Wakristo ni maarufu kwa utajiri na  elimu  ya juu  kuliko tabaka la kati nchini Syria, wamehamia kwa pamoja kutoka nchini ili kuepuka kundi la kigaidi la Daesh (ISIS au ISIL) pamoja na hali mbaya ya kiuchumi nchini Syria. Viongozi wapya wa HTS wamewahakikishia mara kwa mara watu wa Syria na jumuiya ya kimataifa kwamba watawalinda wachache wote, wakiwemo Mashia, Waalawi, Wadruzi, Wakurdi, na wengine. Mohammed al-Bashir, waziri mkuu wa serikali ya HTS, amewahimiza wakimbizi walioko nje ya nchi kurudi nyumbani kwao, akiahidi kuhakikisha haki za dini na madhehebu yote nchini Syria. Hata hivyo, inabakia kuonekana ikiwa Syria, kama viongozi wake wapya wanavyodai, inaweza tena kuwa mahali ambapo wafuasi wa dini na madhehebu zote wanaweza kuishi pamoja. Shirika lisilo la kiserikali la In Defense of Christians, lenye makao yake Washington, hivi karibuni limeelezea wasiwasi kuhusu hatima ya Wakristo nchini Syria. Baadhi ya vyanzo huko Aleppo vimesema kwamba kufuatia kuanguka kwa Bashar al-Assad na kuchukuliwa kwa mji huo na HTS, Wakristo wanaishi kwa hofu na wanashambuliwa sana na uhalifu na uharibifu. Hata hivyo, Kituo cha Mawasiliano ya Amani, shirika lisilo la faida huko New York, hivi karibuni kiliwahoji Wakristo huko Aleppo katika kusherehekea Siku ya Mtakatifu Barbara, ambayo Wakristo wa Mashariki ya Kati huadhimisha. Walisema kwamba mwanzoni mwa kuchukuliwa kwa Syria na HTS, walihisi hofu na wasiwasi, lakini sasa wanaamini hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi, na makanisa yanaendelea na shughuli zao za kawaida. Baada ya kuanguka kwa serikali Assad, kiongozi wa HTS Abu Mohammad al-Julani, alikutana na kiongozi wa Kikristo. Askofu Hanna Jallouf, Askofu wa muda wa Aleppo, aliambia Vatican News kwamba alikutana na al-Julani, ambaye alimwahidi kwamba Wakristo na mali zao hawatadhuriwa na kwamba matakwa yao yote yatatimizwa. mwaka 2015, al Julani alisema katika mahojiano na Al Jazeera kwamba Wakristo, kama watu wa Kitabu, watakuwa na hadhi maalum na wataruhusiwa kutekeleza imani zao, lakini kwa mujibu wa sheria za Kiislamu na kwamba wanatakiwa kulipa Jaziya (kodi maalum). Mwaka 2013, miaka miwili kabla ya mahojiano ya al- Julani na Al Jazeera, Jabhar Al-Nusra , tawi la al-Qaeda nchini Syria, ambalo liliongozwa na al Julani wakati huo, liliwateka nyara watawa 13 wa Kikristo wakati wa mapigano na vikosi vya Assad. Miezi mitatu baadaye, baada ya Qatar kukubali kulipa watekaji nyara dola milioni 16, waliachiliwa. Leo, inaonekana kwamba al Julani amejiondoa kutoka kwa misimamo yake mikali. Mwaka 2016, alionekana kujitenga na al-Qaeda na sasa anajionyesha kama bingwa wa ustahamilivu wa jamii mbali mbali za kidini, kimadhehebu na kikamu.. Katika siku za hivi karibuni, amevua mavazi yake ya kivita na sasa anavaa mavazi rasmi wakati wa mahojiano na waandishi wa habari, akijadili kuanzishwa kwa taasisi za serikali na ugatuzi wa madaraka ili kuunda utofauti nchini Syria. Serikali ya mpito ya Syria inajumuisha tu wanachama kutoka HTS, bila wawakilishi kutoka kwa vikundi vya kidini au vya kisekula isipokuwa Waislamu wa Sunni. Baadhi wanasema si Wakristo tu wanaoogopa hali hii ya kutisha. Hofu hii iko miongoni mwa Wakristo na Waislamu wa Sunni wenye mitazamoa ya wastani, na ikiwa Syria hatimaye itaangukia chini ya serikali ya mtindo wa Taliban, Wakristo watakuwa walengwa wa kwanza, lakini mwishowe, Waislamu wa Sunni wa wastani pia wataathiriwa na mabadiliko haya.

3491238

Kishikizo: syria wakristo Assad
captcha