Mwezi wa Ramadhan utakapoanza mwezi ujao wa Machi, zaidi ya Waislamu bilioni 1.5 kote duniani wataungana kusherehekea mwezi wa kufunga, kutafakari, na kushirikiana kijamii. Ingawa mil ana desturi nyingi za mwezi huu mtukufu zinafanana kote duniani, kama vile matumizi ya taa za mapambo na mizinga ya kufyatua ishara ya kufuturu, kuna baadhi ya desturi ambazo ni maalum kwa tamaduni na maeneo fulani.
Kuanzia Iraq hadi Indonesia, hizi ni baadhi ya desturi za kipekee zinazosherehekewa katika sehemu mbalimbali.
Haq Al Laila
Maarufu katika eneo la Ghuba ya Uajemi, hasa katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), hii ni sherehe ya watoto inayoadhimishwa siku 15 kabla ya kuanza kwa Ramadhain. Katika Haq Al Laila, ambayo ina maana ya "kwa usiku huu", watoto huvaa mavazi ya kitamaduni na hubeba mifuko ya rangi mbalimbali iliyosokotwa kisha hutembea nyumba hadi nyumba wakiimba nyimbo kwa malipo ya karanga na peremende.
Sherehe hizi kwa kawaida huanza baada ya Swala ya Magharibi, ambapo watoto wenye shauku kubwa mara nyingi huimba kwa sauti ya juu badala ya kuimba kwa kawaida, wakitumaini kupata zawadi nyingi zaidi.
Baadhi ya watu wanahusisha asili ya desturi hii na moja ya Ramadhani za kwanza katika Uislamu, wakati Fatima al-Zahra (SA), binti wa Mtume Muhammad (SAW), alipogawa pipi kwa watu wiki mbili baada ya kuanza kwa mwezi huu mtukufu.
Gargee'an na Qaranqasho
Inayofanana na Haq Al Laila lakini huadhimishwa tarehe 15 ya Ramadhani, Gargee’an ni maarufu nchini Iraq, Kuwait, Qatar, Bahrain na sehemu za Saudi Arabia. Kwa mfano, huko Bahrain, sherehe hizi mara nyingi huwa na tamasha lenye vipindi vya mawaidha ya usiku.
Katika sehemu za Saudi Arabia, siku hii pia inajulikana kama Nasfa, ambayo inamaanisha "katikati" kwa Kiarabu, kwani huangukia katikati ya Ramadhani.
Katika Qatar, siku hii inajulikana kama Garangao, huku nchini Oman ikiitwa Qaranqasho.
Nyekar
Kabla ya kuanza kwa Ramadhani kila mwaka, mamia ya Waislamu wa Indonesia husafiri kuelekea makaburi ya mababu na jamaa zao waliotangulia mbele ya haki na kuwaombea dua. Pia hunyunyiza makaburi kwa petals za waridi ili kuwaenzi.
Ibada hii, inayojulikana kama Nyekar, inalenga kuimarisha mafungamano ya kifamilia huku Waislamu wakijiandaa kwa moja ya nyakati takatifu zaidi za mwaka.
Kwa kawaida, Nyekar hufanyika wiki moja kabla ya kuanza kwa Ramadhani.
Padusan
Kwa maana ya "kuoga" katika lahaja ya Kijava, Padusan ni desturi nyingine ya Kiindonesia ambapo Waislamu huenda kwenye chemchemi za asili na maziwa ili kujisafisha kimwili na kiroho kabla ya kuanza kwa Ramadan.
Ibada hii ya kijamii inalenga kuhimiza tafakari binafsi kabla ya mwezi wa kufunga. Inafahamika kuwa ilikuwepo tangu nyakati za kale katika kisiwa cha Java na baadaye ikawa sehemu ya desturi za Kiislamu.
Mheibes
Maarufu nchini Iraq, Mheibes ni mchezo wa zamani unaoaminika kuwa ulianza tangu enzi za Ukhalifa wa Abbasiyah zaidi ya miaka elfu moja iliyopita.
Sasa, huchezwa kwa kawaida wakati wa Ramadhan baada ya futari na hujumuisha timu mbili. Mchezo huanza timu moja inapoficha pete katika mikono ya mmoja wa wanachama wake. Timu pinzani humteua mchezaji mmoja ambaye jukumu lake ni kubaini ni nani anashikilia pete hiyo kwa kusoma lugha ya mwili na sura za uso. Anapewa nafasi moja pekee ya kubashiri.
Kwa kawaida, mchezo huu huchezwa katika mitaa, lakini pia kuna mashindano ya kitaifa yenye sheria maalum kuhusu muda wa kila raundi na idadi ya pointi zinazohitajika kushinda.
Ingawa mara nyingi huchezwa na wanaume hadharani, wanawake pia hushiriki wanapocheza katika mazingira ya faragha. Wakati wa mchezo, nyimbo za kitamaduni huimbwa, na kuimarisha hisia za mshikamano na jamii.
3492006