Msemaji wa jeshi la Yemen ametangaza habari ya kufanyika mashambulizi ya mafanikio dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion huko Tel Aviv, mji mkuu wa wa utawala wa Kizayuni na pia dhidi ya manuwari ya kubeba ndege ya USS Harry Truman ya Marekani kwenye Bahari ya Sham au Bahari Nyekundu.
Kwa mujibu wa Televisheni ya Al-Masirah, Brigedia Jenerali Yahya Saree ametangaza katika taarifa yake kwamba wanajeshi wa Yemen wameupiga kwa makombora Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Jaffa kwa makombora mawili ya balestiki ya Zulfiqar na Palestine 2.
Ameongeza kuwa: "Vikosi vya jeshi la majini, vya makombora na ndege zisizo na rubani vya Yemen vimeitwanga pia manuwari ya kubebea ndege ya USS Harry Truman ya Marekani na meli nyingine kadhaa zilizoandamana nayo katika operesheni nyingine ya makombora na ndege zisizo na rubani."
Jenerali Saree amesema: "Hili lilikuwa ni shambulio la pili dhidi ya meli za Marekani katika Bahari Sham kwenye muda wa saa 24 zilizopita na limeendelea kwa saa kadhaa."
Ameongeza kuwa: "Katika operesheni hii, vikosi vya jeshi la Yemen vimefanikiwa kuzima hujuma ya anga ya adui Mmarekani dhidi ya Yemen."
Vilevile msemaji huyo wa jeshi la Yemen amesisitiza kuwa taifa imara la Yemen litaendeleza operesheni zake za kuzuia meli zote za Israel na zinazoelekea Israel zisipite kwenye Bahari ya Sham kama ambavyo mashambulizi dhidi ya maeneo muhimu ya utawala wa Kizayuni kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu nayo yataendelea ikiwa ni sehemu ya kuliunga mkono taifa la Palestina hasa wakazi wa Ukanda wa Ghaza wanaofanyiwa ukatili wa kuchupa mipaka na Israel.
3492488