IQNA

Muqawama

Jeshi la Yemen lashambulia kwa kombora wizara ya vita ya utawala wa Israel

13:26 - January 14, 2025
Habari ID: 3480052
IQNA-Jeshi la Yemen limetangaza kwamba limeilenga kwa mafanikio Wizara ya Vita ya utawala haamu wa Israel na kuitwanga kwa kombora la balestiki.

Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree, amesema: "Operesheni hiyo imefanikishwa kwa kombora la balestiki la Palestina-2 na limepiga shabaha kwa ustadi wa hali ya juu baada ya mifumo ya ulinzi wa makombora ya utawala wa Kizayuni wa Israel kushindwa kulitungua." 

Ameongeza kwa kuksema: "Kikosi cha makombora cha jeshi la Yemen kimefanya operesheni maalumu na kuipiga Wizara ya Vita ya Israel katika mji wa Jaffa ikiwa ni sehemu ya kuendelea taifa la Yemen kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina na mujahidina shupavu na mashujaa wa Palestina ambao wanaendelea kupambana kiume kujibu jinai za utawala wa Kizayuni."

Msemaji wa jeshi la Yemen ameongeza kuwa: "Hii ni operesheni ya tatu dhidi ya maeneo nyeti na hassasi ya Israel katika muda wa saa 12 zilizopita. Tutaendelea na operesheni zetu hadi Israel itakapokomesha mashambulizi yake na kuacha kuuzingira Ukanda wa Ghaza." 

Katika upande mwingine gazeti la Kizayuni la "Jerusalem Post" limeripoti kuwa, Wazayuni 11 wamejeruhiwa wakati wakikimbilia kwenye mashimo na mahandaki yao kwa kuhofia kombora hilo la Yemen.

Kabla ya hapo vyombo vingine vya habari vya Israel vilikuwa vimeripoti mapema leo asubuhi kwamba ving'ora vya hatari vimesikika vikilia kila mahali.

Vyombo hivyo vimeongeza kuwa, mifumo ya ulinzi wa anga ya Israel ilikuwa imewashwa katika mji wa Tel Aviv na kwamba miripuko mingi imesikika. Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya Israel, walowezi wapatao milioni 2 wamekimbilia kwenye mashimo kwa kuhofia kombora la Yemen.

Jeshi la Yemen limekuwa likiendesha mamia ya mashambulizi dhidi ya Israel tangu tarehe 7 Oktoba 2023, wakati utawala wa Israel ulipoanza kutekeleza vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza chini ya uungaji mkono wa Marekani. Tangu wakati huo hadi sasa Israel imeua Wapalestina zaidi ya 46,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Jeshi la Yemen limesisitiza kuwa litaendelea kuishambulia Israel hadi utawala huo utakapomaliza vita vyake dhidi ya Gaza

3491453

Habari zinazohusiana
Kishikizo: yemen israel palestina
captcha