Mashambulizi hayo, yaliyotekelezwa siku ya Jumatano, yalilenga maeneo muhimu ndani na pembezoni mwa mji mkuu wa Syria, Damascus, pamoja na Suwayda kusini mwa nchi. Vyombo vya habari vya serikali ya Syria viliripoti kuwa angalau watu watatu waliuawa baada ya mashambulizi ya anga kulenga maeneo karibu na Wizara ya Ulinzi na viwanja vya ikulu vilivyo jirani.
Jeshi la Israel lilidai kuwa mashambulizi hayo yalilenga kuzuia vikosi vya Syria, ambavyo walivituhumu kwa kuhatarisha jamii ya wachache wa Druze, kufuatia mapigano yanayoendelea Suwayda kati ya jamii za Druze za eneo hilo na makundi ya Wabedui. Uhasama huo umeongezeka tangu katikati ya mwezi Julai.
Iran imekemea vikali operesheni hizo za kijeshi za Israel nchini Syria, ikizitaja kuwa mwendelezo wa mienendo ya kikatili na inayotarajiwa ya utawala huo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ametoa wito wa juhudi za pamoja za kikanda na kimataifa kukomesha kile alichokiita uchokozi usiodhibitiwa wa Israel.
"Utawala wa Israel, uliojaa ghadhabu, hauna mipaka na huelewa lugha moja tu. Dunia, ikiwemo eneo hili, lazima iungane kukomesha uchokozi wake usio na kifani," aliandika Araghchi kupitia X. Alisisitiza msimamo thabiti wa Iran katika kuunga mkono uhuru wa Syria, mamlaka yake kamili ya kitaifa, na mshikamano na wananchi wa Syria.
Russia imesema, mashambulio ya karibuni yaliyofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Syria yanastahili kulaaniwa "vikali".
Taarifa iliyotolewa leo na Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema: "mashambulizi haya, ambayo yanajumuisha ukiukaji mkubwa wa uhuru wa nchi na sheria ya kimataifa, yanastahili kulaaniwa vikali".
Huku ikiielezea mivutano ya karibuni iliyozuka nchini Syria kuwa ni ya 'kutia wasiwasi mkubwa sana' taarifa hiyo imesema, Moscow inatumai utekelezwaji wa hatua za kupunguza hali hiyo utasaidia kupunguza mvutano na kuleta utulivu nchini humo.
Aidha, taarifa hiyo imesema Russia inaamini kuwa njia ya kusuluhisha mivutano hiyo ni kupitia mazungumzo na "kuimarisha mwafaka wa kitaifa, kuheshimu haki za wawakilishi wote na jamii za makundi mseto ya watu wa Syria."
Wizara ya mambo ya nje ya Russia imeongeza kuwa, Moscow inatilia mkazo msimamo wake thabiti kuhusiana na haja ya kuheshimiwa uhuru, umoja na ardhi yote ya Jamhuri ya Kiarabu ya Syria.
Malengo ya Israel
Malengo ya utawala wa kizayuni katika kuzusha mgogoro nchini Syria ni pamoja na kuzidisha tofauti za kidini na kikabila ili kuzusha vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe, kukabiliana na uthabiti wa kisiasa na kukwamisha mchakato wa amani na pia makubaliano yoyote ya kisiasa yatakayopelekea utulivu wa ndani nchini Syria. Utawala wa Kizayuni umekuwa ukitumia uungaji mkono wa Marekani hususan katika siku za hivi karibuni kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la malengo yake maovu nchini Syria.
Malengo ya utawala wa Kizayuni katika kuishambulia Syria ni pamoja na kupanua ardhi yake, kudhoofisha kabisa uwezo wa kiulinzi wa nchi hiyo, kutumia vibaya ukosefu wa utulivu wa ndani wa Syria, na kuweka mazingira ya kushinikiza kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Tel Aviv. Malengo hayo yamepangwa ndani ya fremu ya stratijia ya muda mrefu ya utawala wa Kizayuni ya kuongeza ushawishi wa utawala huo, Marekani na Magharibi katika eneo.
Nchi za eneo na ulimwengu wa Kiislamu kupitia uratibu na umoja zinaweza kuzima njama mbaya za mhimili wa Marekani-Uzayuni za kuzusha mgogoro katika eneo ikiwemo Syria.
Hatua za utawala wa Kizayuni katika eneo ambazo bila shaka zinatekelezwa kwa uungaji mkono wa Marekani, zimekuwa sehemu ya matukio yaliyoanza miaka kadhaa iliyopita kwa hujuma za kijeshi za Marekani na washirika wa Magharibi wa White House dhidi ya Iraq na Afghanistan, na kuweka msingi wa kuzusha mgogoro wa kiusalama na ukosefu wa utulivu katika eneo hili.
3493878