Sherehe ya kuwaaga Mahujaji watarajiwa ilifanyika Jumatatu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Kulingana na Duale, jumla ya Wakenya 3,300 mwaka huu wataelekea Makka kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hija.
"Leo asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi, niliaga kundi la kwanza la watu 300 wanaoelekea Saudi Arabia kwa ajili ya Hija" Duale alisema kupitia mtandao wa kijamii wa X.
Duale alitoa shukurani zake kwa vyombo mbalimbali kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha utaratibu mzuri wa safari kwa mahujaji
Aliishukuru serikali kwa kurahisisha maombi na utoaji wa hati za kusafiria kupitia Idara ya Uhamiaji ya Kitaifa.
Aidha alishukuru Baraza Kuu la Waislamu wa Kenya (SUPKEM) na Ubalozi wa Saudi nchini Kenya kwa kuhakikisha utoaji wa visa zaHija kwa wakati unaofaa.
Walioshiriki katika sherehe hiyo ya kuwaaga wanaoelekea Hija alikuwemo mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Kenya, Supkem, Al Hajj Hassan Ole Nado na Naibu Balozi wa Saudi nchini Kenya, Nassir Alfuraidy.