IQNA

Waislamu Kenya watakiwa kuungana kukabiliana na ubaguzi

0:04 - April 19, 2014
Habari ID: 1396701
Viongozi wa Kiislamu nchini Kenya wamewataka raia wa nchi hiyo kuwa na umoja na mshikamano. Viongozi hao wamekutaja kudumishwa umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi kuwa ni jambo muhimu la lenye udharura.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Sheikh Ibrahim Lithome ambaye ni miongoni mwa viongozi wa Waislamu Kenya pia amesema kwamba, kushadidi hitilafu za ndani kunawanufaisha wanamgambo wenye mfungamano na kundi la al Shabab na kueleza kuwa Waislamu wamo katika kipindi nyeti sasa na kwamba jamii hiyo inapasa kutoa mchango wake mkubwa katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Watu wengi huko Kenya wanaamini kuwa Waislamu nchini humo wanalengwa katika mapambano dhidi ya ugaidi. Fikra hii imepata nguvu zaidi baada ya operesheni kubwa ya msako iliyofanywa na vyombo vya usalama vya Kenya dhidi ya eneo la Eastleigh lenye raia wengi Wasomali. Wanaharakati wa masuala ya kiuchumi pia wamepanga kufanya maandamano makubwa ili kulalamikia miamala mibovu ya polisi. Hata hivyo maafisa wa polisi wa Kenya wanasisitiza juu ya kuendelezwa operesheni za kiusalama katika eneo hilo. Operesheni hiyo ilianza tarehe Pili mwezi huu baada ya mlipuko uliouwa na kujeruhi watu kadhaa.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa kushadidi hitilafu kati ya Waislamu na Wakristo katika maeneo mbalimbali ya Afrika, kunazinufaisha nchi wakoloni na kuhalalisha uingiliaji haramu wa nchi hizo katika masuala ya Afrika. Awali kuuawa kwa makhatibu wa Kiislamu katika mji wa pwani wa Mombasa na huko mashariki mwa Kenya, kulipelekea kuzuka mapigano makali nchini humo. Wafuasi wa makhatibu hao waliyataja mauaji hayo kuwa ni kinyume cha sheria na kusema kuwa viongozi wa serikali wamehusika katika mauaji hayo.

Kwingineko Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amekutana na wabunge kutoka eneo la kaskazini mashariki lenye wakaazi wengi wa kabila la Somali na kuwahakikishia kuwa jamii yao haitalengwa katika oparesheni za usalama nchini humo.

Jumatano Rais Kenyatta alikutana na wabunge 25 Waislamu wakiongozwa na kiongozi wa waliowengi bungeni Aden Duale. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu wa Rais William Ruto, Inspekta Mkuu wa Polisi David Kimaiyo na Katibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Mutea Iringo.

Rais Kenyatta amewafahamisha Wabunge hao na kuwahakikishia kuwa oparesheni zinazoendelea za usalama hazilengi jamii yoyote na kwamba zitafanyika kwa mujibu wa sheria.  Baada ya kikao hicho, Duale amezungumza na waandishi habari na kusema, 'Rais amewahakikishia viongozi wa jamii ya Wasomali na Waislamu kuwa hawatalengwa katika msako unaoendelea na kwamba serikali itashirikiana na wenyeji katika hatua za usalama.'

Huu ni mkutano wa pili wa Rais Kenyatta na viongozi Wasomali tokea oparesheni za usalama zianze wiki chache zilizopita baada ya kutokea hujuma za kigaidi katika miji ya Nairobi na Mombasa. Vikosi vya usalama vya Kenya vinalaumiwa kuwalenga Waislamu na hasa wenye asili ya Kisomali katika oparesheni za kuwasaka wafuasi wa kundi la kigaidi la Al Shabab.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa kuwepo mipaka mirefu kati ya Kenya na Somalia kunaifanya Kenya iathiriwe na matukio ya Somalia.

Kwa sasa kundi lenye misimamo ya kufurutu ada la al Shabab ndilo linalohusika na mgogoro wa ndani wa Somalia na nchi jirani. Kundi hilo linaonekana kuanza kujipanga upya licha ya kupata kipigo kikali cha askari wa kimataifa na kieneo walioko huko Somalia. Hata hivyo machafuko ya hivi karibuni huko Somalia na nchi jirani kama Kenya yanazusha maswali kwamba kundi hilo la al Shabab linapata silaha na misaada mingine kutoka wapi? Ni nani anayedhamini na kulifadhili kundi hilo?

Wataalamu wa mambo wanasema machafuko ya sasa katika eneo la Pembe ya Afrika yanazifaidisha nchi za Magharibi na yanatumiwa kama kisingizio cha kutuma majeshi ya nchi hizo katika eneo hilo la kistratijia.

1395707

Kishikizo: kenya waislamu somalia
captcha