IQNA

Mashindano ya ۳۱ ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yamalizika Tehran

18:48 - June 02, 2014
Habari ID: 1413796
Mashindano ya ۳۱ ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yamemalizika leo Jumatatu hapa Tehran bada kuendelea kwa muda wa wiki moja.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari za Qur’an la Kimataifa IQNA, Mashindano hayo yalianza tarehe 27 Rajab katika mkesha wa maadhimisho ya kubaathiwa Mtume Muhammad SAW. Mashindano hayo yalikuwa na maqarii na mahufadh 120 wa Qur'ani Tukufu kutoka nchi 75 duniani huku kukiwa na jopo la majaji 15 ambapo 10 kati yao ni kutoka nchi za kigeni na watano ni Wairani. Kulikuwa na washiriki kadhaa kutoka nchi za Afrika Mashariki ambapo mashiriki kutoka Tanzania ameshika nafasi ya tano katika qiraa. Makundi yote mawili ya hifdhi na qiraa yalikuwa na washindi watano kila moja. Katika upande wa Qiraa mshindi alikuwa Ja'afar Fardi kutoka Iran huku nafasi ya pili ikishikwa na Mohammad Asghari kutoka Ufilipino akifuatiwa na Mahmoud Mohammad Yusuf Misri naye Sayyid Thamaruddin Samaddof kutoka Tajikistan ameshika nafasi ya nne huku Ustadh Mohammad Ramadhani Iddi kutoka Tanzania akishika nafasi ya tano. Katika kiwango cha hifdhi Behzad Hizhbery kutoka kutoka Iran ameshika nafasi ya kwanza akifuatiwa na Abdulqadir Abdul Aziz Ahmad Abdul Aziz kutoka Misri naye Mutiullah Mutmain kutoka Afghanistan amepata nafasi ya tatu ambapo Mohammad Lotfi Suleiman wa Indonesia ameshika nafasi ya nne huku Haroun Mamadou Hassan wa Niger ameshika nafasi ya tano. Washindi wote wamemtunukiwa zawadi ya Qur'ani Tukufu, Cheti cha Shukrani, nishani na kitita cha fedha. Akizungumza na IQNA, Ustadh Mohammad Ramadhani Iddi kutoka Tanzania amepongeza maandalisi ya mashindano ya mwaka huu na kusema yalikuwa ya kiwango cha juu kabisa. Aidha ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa juhudi zake za kuendeleza harakati za Qur'ani duniani. Ustadh Iddi amesema mashindano ya kimataifa ya Qur'ani hapa Tehran ni mojawapo ya njia muafaka zaidi za kuleta umoja baina ya Waislamu wa maeneo mbali mbali duniani.

1413344

captcha