IQNA

Qur'ani Tukufu yatafsiriwa kwa lugha ya Kiluo

21:43 - July 08, 2016
Habari ID: 3470440
Huku Waislamu duniani wakisherehekehea siku kuu ya Idul Fitr, msomi wa Kiislamu Kenya ameitunukia jamii ya Waluo Qur'ani Tukufu iliyotafsiriwa (tarjumiwa) kwa lugha ya Kiluo.
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Sheikh Omar al Bashir ameifasiri kikamilifu Qur'ani Tukufu kutoka Kiarabu hadi Kiluo, kwa mara ya kwanza katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.

Tarjama hiyo tayari imeshaidhinishwa na Baraza Kuu la Waislamu nchini Kenya, SUPKEM.

Katika mahojiano na Televisheni ya K24, Profesa Bashir ambaye amesomea Uislamu nchini Misri amesema tarjama hiyo itawasaidia Waluo Waislamu ambao hawaifahamu lugha ya Kiarabu. Aidha amesema kutokana na kuwa Waluo wengu hawafahamu vizuri Kiswahili Qur'ani kwa lugha ya Kiluo itawasaidia kuufahamu Uislamu. Ameongeza kuwa tarjama mpya ya Qur'ani kwa Kiluo pia itawasaidia wasio kuwa Waislamu kufahamu Ujumbe wa Uislamu. Profesa Bashir ameongeza kuwa ufahamu wake wa lugha mbili za Kiarabu na Kiluo ni jambo ambalo limekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha kazi yake hiyo yenye umuhimu mkubwa.

Tarjama hiyo ya kwanza ya Qur'ani kwa lugha ya Kiluo inatarajiwa kuzinduliwa Jumamosi hii huko Kendu bay eneo la magharibi mwa Kenya lenye waluo wengi.

Kiluo (au Kijaluo) ni lugha ya Kiniloti nchini Kenya na pia Tanzania inayozungumzwa na Waluo na inakadiriwa kuwa na wazungumzaji karibu milioni sita.
3460327

captcha