IQNA

Al-Azhar: Abdul Basit Alikuwa Balozi wa Qur’ani

16:40 - December 04, 2025
Habari ID: 3481613
IQNA – Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar nchini Misri kimemuelezea marehemu qari mashuhuri Ustadh Abdul Basit Abdul Samad kuwa balozi wa Qur’ani Tukufu.

Katika ujumbe uliotolewa kupitia ukurasa wa Facebook kwa kumbukumbu ya kifo chake, Al-Azhar ilikumbusha wasifu wa qari huyu maarufu, ikisisitiza kuwa alikuwa miongoni mwa maqarii mashuhuri zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu, mwenye “koo ya dhahabu” katika usomaji, na alisafiri Mashariki na Magharibi akiwa balozi wa Qur'ani Tukufu.

Al-Azhar ilieleza kuwa Abdul Basit alizaliwa Januari 1927 katika kijiji cha Al-Mara’za, kitongoji cha mji wa Armant, jimbo la Qena, na alifariki tarehe 30 Novemba 1988.

Qari huyu alipokea mialiko mingi kutoka duniani kote kusoma Qur’ani katika hafla mbalimbali. Alikubali mialiko hiyo na kusafiri sana, akitembelea nchi kama vile Saudi Arabia, Palestina, Syria, Kuwait, Iraq, Morocco, Lebanon, Algeria, Indonesia, Afrika Kusini, Marekani, Ufaransa, India na nyinginezo.

Alisoma Qur’ani katika Misikiti Miwili Mitukufu ya Makka na Madina, jambo lililompa jina la heshima “Sauti ya Makka”. Pia alisoma katika Msikiti wa Al-Aqsa mjini Al-Quds na Msikiti wa Umawi mjini Damascus.

Al-Azhar iliongeza kuwa Abdul Basit aliheshimiwa na wafalme na marais, waliompokea kwa heshima kubwa na mapokezi ya kifahari.

Aidha, alitunukiwa medali na heshima nyingi za kimataifa, zikiwemo Medali ya Cypress kutoka Jamhuri ya Lebanon, Medali ya Dhahabu ya Pakistan, Medali ya Wanazuoni kutoka kwa Rais wa Pakistan wa wakati huo, Zia-ul-Haq, Medali ya Heshima ya Senegal, tuzo kutoka Jamhuri ya Syria na serikali ya Malaysia, Medali ya Redio ya Misri katika maadhimisho ya miaka 50, na Medali ya Heshima ya Misri.

Ni vyema kutaja kuwa Jumapili iliyopita, Wizara ya Awqaf ya Misri ilikumbuka kumbukumbu ya kifo cha qari huyu mkubwa wa Misri.

3495607

captcha