Hujjatul Islam Hamid Reza Arbabsoleimani, Naibu Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu Iran anayesimamia Masuala Qur’ani na Ahlul Bayt (Etrat) , alitoa kauli hiyo alipokutana na kundi la wanaharakati wa Qur’ani kutoka Thailand, mjini Tehran.
Akasema, “Ikiwa kweli tunatamani afya na wokovu wa jamii ya kibinadamu, basi hakuna njia nyingine ila kurejea katika Qur’ani. Qur’ani ndiyo mwongozo wa hakika wa maisha.”
Aliongeza kuwa, “Ikiwa sisi ni wahudumu wa Qur’ani, tunapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hii. Tumeongozwa katika njia hii, na ni wajibu wetu kuongeza uelewa wetu wa maana za Qur’ani na kuzitekeleza katika maisha ya kila siku.”
Arbabsoleimani aliendelea kwa kusema, “Kazi yetu ya pamoja nanyi ni Qur’ani Tukufu, lugha ya pamoja ya Waislamu duniani. Qur’ani ni ramani ya kimkakati ya maisha yetu ya sasa na ya baadaye. Harakati yenu kubwa ya kueneza na kukuza utamaduni wa Qur’ani ni juhudi adhimu na ni baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.”
Aliwahimiza wanaharakati wa Qur’ani kushikamana na Swala, akisisitiza kuwa Qur’ani imetilia mkazo sana ibada hii.
“Mkiwa mabalozi wa Qur’ani, someni aya za Mwenyezi Mungu kwa ufasaha, zifanyieni kazi kwa ikhlasi, na mzieneze kwa hekima. Dunia ya leo ina kiu ya maarifa ya Qur’ani. Pazia la ujinga na kughafilika limewazuia watu kunufaika na nuru ya Qur’ani. Sisi sote tunapaswa kujitahidi kuliondoa pazia hili, tupambane na ujinga na ushirikina, ili nuru ya Qur’ani iwake mioyoni mwa watu. InshaAllah, siku itafika ambapo bendera ya Qur’ani itainuliwa kila kona ya dunia.”
Katika mkutano huo, aligusia pia ziara ya kundi hilo katika maeneo matukufu ya Kiislamu nchini Iran, na kusema: “Ziara yenu katika miji mitakatifu ya Mashhad na Qom, pamoja na kutembelea makaburi ya watu wa nyumba ya Mtume (Ahlul Bayt), ni ishara kuwa safari hii imekuwa yenye baraka na mafanikio kwenu.”
Alisema kuwa mahusiano ya Qur’ani kati ya Iran na Thailand yatazidi kuimarisha ushirikiano wa shughuli za Qur’ani baina ya mataifa haya mawili.
Katika mkutano huo, Mkuu wa Kituo cha Uratibu wa Kiutamaduni cha kusini mwa Thailand aliwasilisha ripoti kuhusu shughuli za Qur’ani katika eneo hilo.
Akimshukuru kwa ukarimu wa watu wa Iran, aliomba kuwepo kwa miradi ya pamoja ya Qur’ani kati ya mataifa hayo mawili.
Chakrapong Abi Mahatham alieleza kuwa asilimia 90 ya wakazi wa kusini mwa Thailand ni Waislamu, na bajeti kubwa imetengwa kwa ajili ya shughuli za Qur’ani.
Kwa sasa, vituo 15 vya shughuli za Qur’ani vimeanzishwa katika eneo hilo, alisema.
Mwanaharakati huyo wa Qur’ani kutoka Thailand alimkaribisha rasmi afisa huyo wa Iran kutembelea makumbusho ya Qur’ani katika kusini mwa Thailand, na alipendekeza kuandaliwa kwa maonesho ya pamoja ya Qur’ani kati ya Iran na Thailand.
3493336