IQNA

Mwana wa Abdul Basit asifu uzinduzi wa Jumba la Makumbusho la Maqari wa Qur’an nchini Misri

10:29 - January 08, 2026
Habari ID: 3481782
IQNA – Mwana wa qari maarufu wa Misri aliyefariki, Abdul Basit Abdul Samad, amepongeza kuanzishwa kwa Jumba la Makumbusho la Waqari wa Qur’an nchini humo.

Sheikh Tariq Abdul Basit alisema jumba hilo ni heshima ya kiroho kwa maqari waliolihifadhi Qur'ani Tukufu kwa sauti zao, gazeti la Al-Dustur liliripoti. Alibainisha kuwa mradi wa kuanzisha jumba hilo ni hatua chanya na muhimu ya serikali, iliyotekelezwa kwa ushirikiano wa wizara za Awqaf na Utamaduni.

“Kukusanya vitu binafsi vya maqari mashuhuri na kuviweka katika jumba maalumu ni heshima ya kiroho kwao, kwani walihifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa sauti zao. Ni jambo la kimaumbile kuwa wasifu na mali zao zihifadhiwe katika mahali panapolingana na hadhi yao,” alisema Sheikh Tariq. Aliongeza kuwa serikali na wote walioshiriki wanastahili pongezi kwa mradi huu mkubwa. “Huu ni mradi muhimu wa kitamaduni na kidini unaowawezesha wananchi wa ndani na nje ya Misri kujifunza kuhusu wasifu wa waqari wakubwa na kuzijua maisha yao kwa karibu zaidi.”

Kuhusu michango ya familia za waqari, Sheikh Tariq alisema kuwa kwa kuzingatia thamani ya kiroho ya vitu hivyo, haikuwa kazi rahisi kwa familia kuviachia. Lakini dhamana ya taasisi yenye kuaminika kuhifadhi na kuonyesha mali hizo kwa heshima na usalama ndiyo iliwatia moyo kukubali. Alieleza kuwa vitu hivyo vilikuwa vimehifadhiwa na familia kwa miaka mingi, kila mmoja akibeba kumbukumbu kama picha, sauti au kitu binafsi. Lakini kuviweka katika jumba rasmi kunahakikisha vizazi vijavyo vitavihifadhi na watu watapata fursa ya kufahamu historia ya maisha ya waqari hao.

Sheikh Tariq alieleza hisia zake alipotembelea jumba hilo: “Nilipoingia ndani, niliona aya za Qur’an zimechongwa ukutani pande zote na nikahisi kama niko bustani ya peponi. Nilijawa na mshangao na heshima, na wakati huo huo nikahisi amani na furaha, kwa kuwa hili ni alama kubwa ya kidini na kitamaduni ambayo kila Mwislamu anajivunia.” Alisema daima aliota kuwa na mahali pa kuhifadhi urithi huu, lakini hakuwahi kufikiria kuwa lingekamilika kwa uzuri na umaridadi wa aina hii.

Jumba la kwanza la maqari wa Qur’an lilifunguliwa katikati ya Desemba 2025 katika Kituo cha Kitamaduni na Kiislamu cha Misri kilichopo Mji Mkuu Mpya karibu na Cairo. Linahifadhi kazi binafsi za maqari 11 wakubwa wa Misri, akiwemo Muhammad Rifa’at, Abdul Fattah Shasha’ei, Taha Al-Fashni, Mustafa Ismail, Mahmoud Khalil Al-Husari, Muhammad Siddiq Minshawi, Abu al-Ainain Shuaisha, Mahmoud Ali Al-Banna, Abdul Basit Abdul Samad, Muhammad Mahmoud Tablawi, na Ahmed Al-Ruzifi. Familia za maqari hawa walihudhuria sherehe ya ufunguzi. Jumba hilo lilibuniwa na mhandisi Karim Al-Shapouri na lina kumbi nne kuu zenye mkusanyiko wa maandiko, kazi adimu na leseni za Qur’an zilizotolewa na Al-Azhar. Pia lina ukumbi maalumu wa kusikiliza tilawa zilizoteuliwa, unaowapa wageni tajiriba ya kina ya kujifunza zaidi kuhusu waqari na kusikiliza sauti zao.

3495993

Habari zinazohusiana
captcha