IQNA

Wana wa Sheikh Abdul Basit wahudhuria uzinduzi wa Apu ya Al Moeen Sharjah, UAE

16:01 - January 23, 2026
Habari ID: 3481837
IQNA – Aplikesheni mahiri ya “Al Moeen” imezinduliwa katika hafla maalumu iliyofanyika Alhamisi katika Chuo cha Qur’ani Tukufu mjini Sharjah, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Sheikh Sultan Bin Mohammed Al Qasimi, mjumbe wa Baraza Kuu na Mtawala wa Sharjah, pamoja na wana wa marehemu qari mashuhuri wa Misri, Sheikh Abdul Basit Mohammed Abdul Samad, walihudhuria hafla hiyo iliyokuwa na uzito wa kiroho na kihistoria.

Mtawala wa Sharjah aliwakaribisha wageni kwa heshima kubwa na akatoa kauli ya fahari kuhusu hadhi ya kipekee ya Sheikh Abdul Basit Abdul Samad, akisisitiza mchango wake wa kudumu katika kuhudumia Qur’ani Tukufu na sanaa ya tilawa ambayo imevuka vizazi na mipaka ya ulimwengu wa Kiislamu.

Alisisitiza kupata kwa Sheikh Abdul Basit vyeti vya usomaji wa Qur’ani katika qira’a saba, pamoja na athari ya kina aliyoiacha katika nyoyo za Waislamu duniani kote—athari inayobaki hai katika misikiti, majukwaa ya Qur’ani na nyoyo za wasikilizaji wa mwambao na bara.

Sheikh Sultan alithibitisha kuwa Emirati ya Sharjah inaendelea kuunga mkono miradi na juhudi zote zinazolenga kuhudumia Qur’ani Tukufu na sayansi zake, akionyesha dhamira ya kuendeleza urithi wa Kiislamu kwa njia yenye mizizi na inayofungamana na wakati.

Alisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia za kisasa kuhifadhi turathi za Qur’ani na kuziwasilisha kwa vizazi vijavyo, kwa namna inayokuza maadili bora ya Kiislamu, inayoendana na roho ya zama hizi, na inayoakisi dhamira ya kitamaduni na kibinadamu ya Sharjah kama kitovu cha elimu, ustaarabu na mwanga wa Kiislamu katika Ghuba ya Uajemi.

Wana wa Sheikh Abdul Basit walitoa shukrani na pongezi zao kwa Mtawala wa Sharjah kwa mapokezi ya heshima na kwa kuthamini wanatilawa mashuhuri wa Qur’ani.

Habari inayohusiana:

Baadaye, Sheikh Sultan alitembelea Makumbusho ya Maqari Mashuhuri katika Chuo hicho, ambako alizindua sehemu maalumu iliyotengwa kwa ajili ya vitu binafsi vya Sheikh Abdul Basit Mohammed Abdul Samad. Maonyesho hayo yanajumuisha mkusanyiko wa picha na vitu vya kumbukumbu vinavyoonyesha safari ya maisha ya Sheikh, mikutano yake na wanazuoni, viongozi wa serikali, na watu mashuhuri wa kimataifa.

Sheikh Sultan pia alitazama makala ya video ya kihistoria iliyoangazia vipengele vya malezi ya Sheikh, safari yake ya maisha, mwanzo wa safari yake katika ulimwengu wa tilawa ya Qur’ani, na mchango wake mkubwa katika kuhudumia Qur’ani Tukufu.

Sheikh Sultan alisikiliza maelezo ya kina kuhusu maonyesho hayo, yakiwemo misahafu, gramafoni na vifaa vya kurekodia sauti vilivyoachwa na marehemu Sheikh, pamoja na mkusanyiko wa barua zake binafsi alizoandika kwa mkono, cheti chake cha uithibitisho wa qira’a, na medali mbalimbali alizotunukiwa kutoka nchi tofauti duniani.

Abdul Basit’s Sons Attend Launch of Al Moeen App in UAE’s Sharjah

Sheikh Sultan kisha aliwakabidhi wana wa Sheikh Abdul Basit Mohammed Abdul Samad cheti cha kuthamini mchango wao, kwa kukubali kukabidhi mali adimu za baba yao kwa Makumbusho ya Waqari Mashuhuri katika Chuo cha Qur’ani Tukufu. Aliisifu hatua yao ya ukarimu, akisema kuwa itakuwa urithi wa kudumu unaohifadhi mchango wa kipekee wa Sheikh katika kuhudumia Qur’ani Tukufu.

Aidha, Sheikh Sultan alipokea zawadi ya ukumbusho kutoka kwa wana wa Sheikh Abdul Basit Abdul Samad, ambao walitoa shukrani na pongezi zao kwa juhudi zake endelevu katika kuhudumia Qur’ani Tukufu na kuenzi wanatilawa wake mashuhuri.

Habari inayohusiana:

Kisha Sheikh Sultan alizindua aplikesheni mahiri ya “Al Moeen” kwa kubofya kifaa cha kidijitali. Programu hii ni Qur’ani mahiri ya kisasa inayotumia teknolojia mpya za akili mnemba (AI) ikilenga kuwawezesha watumiaji kusoma na kuhifadhi Qur’ani Tukufu kupitia mbinu shirikishi ya hali ya juu.

Sheikh Sultan alitazama mwasilisho la kuona lililoangazia vipengele muhimu vya aplikesheni ya “Al Moeen”, inayochanganya usahihi wa kielimu na urahisi wa matumizi. Inatoa huduma ya tilawa mahiri inayotumia teknolojia ya juu ya utambuzi wa sauti kufuatilia usomaji kwa wakati halisi, kubaini makosa ya matamshi na mahala pa kutamka herufi, na kutoa mrejesho wa marekebisho papo hapo.

Abdul Basit’s Sons Attend Launch of Al Moeen App in UAE’s Sharjah

Aplikesheni hii pia ina modi za kuhifadhi na kurudia kwa akili mnemba, zinazounda mpango wa kuhifadhi kulingana na kiwango cha uwezo wa mtumiaji. Aidha, inatumia mpangilio wa kurasa wa Uthmani, ili kuhakikisha usahihi na ulinganifu na misahafu iliyochapishwa.

Aplikesheni ya “Al Moeen” inaunga mkono utafutaji wa hali ya juu kwa maandishi au sauti, pamoja na violesura vya lugha nyingi, tafsiri na ufafanuzi. Inapatikana kwa Kiarabu, Kiingereza, Kifaransa na Kiurdu, na itapatikana katika maduka ya aplikesheni kwenye vifaa mbalimbali vya kielektroniki hasa simu za mkono, hivyo kuifanya ifae kwa watumiaji kote duniani.

3496151

Habari zinazohusiana
captcha