IQNA

Kijana Muirani Asema Qur’ani Tukufu mempa Nguvu ya Kusomea Udaktari

21:16 - December 06, 2025
Habari ID: 3481622
IQNA – Milad Asheghi, mhifadhi kamili wa Qur’ani Tukufu na mwanafunzi wa mwaka wa mwisho wa udaktari kutoka Tabriz, Iran, amesema Qur’ani Tukufu imekuwa nguvu thabiti iliyomwongoza kupitia changamoto za masomo ya udaktari.

Akiwa amezaliwa Januari 22, 2000, Asheghi alihifadhi Qur’ani nzima akiwa na umri wa miaka kumi. Anasema safari yake ilianza kwa msaada wa wazazi wake, hususan mama yake, na ikaendelea kwa uhusiano wa kina na wa makusudi zaidi na Qur’ani alipokuwa akikua. “Nilikuja kuelewa kuwa heshima ambayo Qur’ani humpa mtu ni kubwa kuliko cheo au nafasi yoyote,” alisema. “Nilihisi baraka zake katika nyakati ngumu zaidi za masomo yangu, wakati wa msongo na uchovu.”

Asheghi anaamini vyuo vikuu vina jukumu muhimu katika kulea wanafunzi ambao ni imara kielimu na kiroho. Anasema walimu wenye malezi na maarifa ndiyo msingi muhimu zaidi wa malezi hayo. “Wakati profesa mwenye uzoefu wa miongo kadhaa anasimama kwa heshima ya Qur’ani, hilo linatoa ujumbe wenye nguvu kwa wanafunzi,” alisema.

Alibainisha kuwa wanafunzi hunawiri wanapohisi wamesaidika katika maendeleo yao ya kielimu na kiroho. Akijibu hoja kwamba kushiriki katika Qur’ani huenda kukawazuia wanafunzi kielimu, Asheghi alikataa dhana hiyo. Alisisitiza umuhimu wa kuonyesha mifano halisi ya wanafunzi wanaofanikiwa katika taaluma ngumu huku wakiendelea kushiriki katika duru za Qur’ani. “Wakati wanafunzi wanamuona mtaalamu wa tiba au uhandisi ambaye pia ni Hafidh wa Qur’ani, hutambua kuwa inawezekana kutembea njia zote mbili,” alisema. Alikumbuka wenzake kadhaa wakimwambia walihamasika kuanza kuhifadhi kutokana na mfano wake.

Asheghi alisema hujikumbusha mara kwa mara: “Nilihifadhi Qur’ani ili Qur’ani inilinde.” Anaamini Qur’ani humlinda mtu si tu katika masomo, bali pia katika maamuzi ya maisha na nyakati ngumu. “Jamii yetu inahitaji si wasomaji na wahifadhi pekee, bali wale wanaoishi kwa Qur’ani,” aliongeza.

Milad Asheghi amepata heshima kadhaa za kitaifa na kimataifa, ikiwemo nafasi ya pili katika kipengele cha Qur’ani kamili kwenye Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya 9 nchini Uturuki, nafasi ya pili katika Mashindano ya Kitaifa ya Qur’ani ya 48 nchini Iran, na nafasi ya kwanza katika mashindano ya kitaifa ya wanafunzi wa Qur’ani. Pia alishika nafasi ya juu katika mashindano ya kitaifa kwa washiriki walio chini ya miaka 16.

 

/3495629

captcha