IQNA

Redio ya Mauritania yaanza kurekodi qiraa ya tartil ya Qur'ani Tukufu

13:51 - January 21, 2026
Habari ID: 3481831
IQNA-Hafla ya kuanza kurekodi qiraa au usomaji wa Qur’ani Tukufu kwa mtindo wa tartīl kwa riwaya za Warsh na Qālūn imefanyika katika Redio ya Mauritania.

Kwa mujibu wa taarifa ya IQNA ikinukuu Shirika la Habari la Mauritania, qiraa tatu za Qur’ani Tukufu zitarekodiwa mwaka 2026 Miladia (1447 Hijria) kama sehemu ya mpango maalumu wa kutayarisha qiraa ya Qur'ani kwa sauti na video kwa ushirikiano na Idhaa (Radio) ya Qur’ani ya Mauritania na kituo cha setilaiti cha “Mahdhara”.

Katika hafla hii, makari walioteuliwa kushiriki katika mradi wa kurekodi walihudhuria na wakatoa mifano ya tilawa zao kwa riwaya za Warsh na Qalun.

Aidha, Sayyid Ahmad Wald an-Nayni, mshauri wa Rais wa Mauritania; Sayyid Muhammad Abdulqadir Wald A‘ladah, Mkurugenzi Mkuu wa Radio Mauritania; pamoja na baadhi ya viongozi wa kituo hicho na wajumbe wa Baraza la Kisayansi la Radio Qur’ani na kituo cha setilaiti cha Mahdhara walikuwa miongoni mwa waliohudhuria.

Sayyid Muhammad al-Amin Wald at-Talib Uthman, Katibu Mkuu wa Baraza la Kisayansi la Radio Qur’ani Mauritania na kituo cha Mahdhara, alisema kuwa hafla hii ni fursa ya kuangazia juhudi za Radio Mauritania katika kuhudumia Qur’ani na watu wanaojishughulisha na Qur’ani, ambao ni miongoni mwa waja maalumu wa Mwenyezi Mungu.

Habari inayohusiana:

Akaongeza kuwa maqari bora wa mashindano ya awali ya Qur’ani nchini Mauritania, baada ya kupitiwa na kamati maalumu, wamechaguliwa kushiriki katika mradi huu; na kwamba wajumbe wa Baraza la Kisayansi la Radio Qur’ani ambao wanapenda kushiriki katika kurekodi pia wanaweza kujiunga.

Sayyid Shaykh Wald ash-Shaykh Ahmad, mjumbe wa kamati ya kurekodi Qur'ani Tukufu, alisema kuwa hafla hii ni tukio adimu linalowahusu wahifadhi wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na kwamba kujishughulisha na Qur’ani na wahudumu wake kuna mchango mkubwa katika kulinda jamii na kuimarisha umoja na mshikamano wa kijamii.

4329165

captcha