IQNA

Mamia ya Waislamu washiriki hafla ya Iftar katika eneo la Times Square, New York

7:41 - February 24, 2026
Habari ID: 3481982
IQNA – Katika hali ya kiroho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, hafla ya iftar (futura ya kufungua saumu) ilifanyika mwishoni mwa wiki hii katika Times Square, mojawapo ya maeneo mashuhuri na yenye shughuli nyingi zaidi jijini New York.

Mamia ya Waislamu wanaoishi New York walikusanyika pamoja kufungua saumu zao na kuswali Swala ya Taraweeh, wakionyesha mshikamano na uzuri wa Uislamu katikati ya jiji lenye harakati nyingi. Hafla hiyo iliandaliwa kwa mara ya tano mwaka huu na akaunti ya mitandao ya kijamii iitwayo “Wayoflifesq”, iliyowaunganisha wanaume na wanawake kutoka matabaka na asili mbalimbali.

Wakikusanyika katika kona ya Broadway na 7th Street, eneo lenye msongamano mkubwa zaidi Times Square, Waislamu walifungua saumu zao kwa dua na dhikri, mara tu adhana ya Magharibi ilipoingia. Kwa ajili ya futari, pakiti za chakula bila malipo ziligawiwa kwa takribani watu 1,500.

Vilevile, nakala 1,200 za Qur’ani Tukufu ziligawiwa kwa washiriki na watu waliokuwapo katika eneo hilo. Mmiliki wa akaunti ya Wayoflifesq, anayejulikana kwa jina la “SQ”, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mara nyingi Uislamu huwasilishwa vibaya katika vyombo vya habari vya Magharibi.

Alisema: “Lengo letu hapa ni kuwaelezea watu Qur’ani, kuwaelimisha, na kuujulisha ulimwengu kuhusu Uislamu.”

Akaongeza kwa sauti ya mwaliko na undugu: “Tunataka muungane nasi na mfahamu kuwa utamaduni wetu ni utamaduni wenu pia. Njooni mketi nasi. Njooni mle nasi. Njooni mfungue saumu nasi na mfurahe uzuri wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.”

Harman, mmoja wa wajumbe wa timu ya maandalizi, alisema: “Hii ni New York, kila wakati kuna jambo linaendelea. Watu hushangaa wanapopita na kuona kinachoendelea. Leo tumegawa nakala 1,200 za Qur’ani. Watu wanazichukua kwa Kiingereza, Kihispania, Kijerumani, kwa lugha yoyote wanayoihitaji.”

Baada ya kufungua saumu, kundi hilo lilitekeleza Swala ya Magharibi, kisha Ishaa na Taraweeh juu ya mikeka waliyoileta, chini ya taa za Times Square, licha ya hali ya hewa ya baridi na mvua nyepesi.

Hafla ya iftar na swala hizo ilivutia hisia kubwa kutoka kwa wakazi wa New York na watalii waliokuwapo, wengi wao wakirekodi tukio hilo kwa simu zao za mkononi wakati wa swala.

Katika tukio hilo lenye baraka, watu wawili waliingia katika Uislamu kwa kutamka Shahada. Polisi wa New York walichukua hatua madhubuti za kiusalama kuhakikisha usalama wa washiriki wote.

Inafahamika kuwa hafla ya kwanza ya iftar katika Times Square ilifanyika mwaka 2022, na tangu wakati huo imekuwa alama ya kuonesha uso wa amani, ukarimu na mwaliko wa Uislamu katikati ya jamii ya kimataifa.

4336147

captcha