
Hafla hiyo ilifanyika siku ya Jumamosi, tarehe 16 Mei, ikiandaliwa na Sakina Förlag (Shirika la Uchapishaji la Sakina) kama sehemu ya mradi wa kimataifa kwa kushirikiana na Taasis ya Restu, kwa mujibu wa taarifa ya tovuti ya Alkompis.
Wawakilishi wa balozi za nchi za Kiarabu na Kiislamu walioko Uswidi, pamoja na viongozi wa jumuiya na taasisi za Kiislamu, walihudhuria hafla hiyo.
Pembeni ya tukio hilo pia kulifanyika maonesho ya maandiko ya Kiislamu na sanaa za kiislamu, yakionyesha uzuri wa turathi za Kiislamu na kaligrafia ya Kiarabu.
Qais Ataullah, afisa wa Sakina Förlag, alisema katika hafla hiyo kwamba wazo la mradi huu lilianza kwa namna ya kawaida mnamo mwaka 2007 kupitia ukurasa wa mitandao ya kijamii, uliokuwa na lengo la kununua nakala za tafsiri ya Qur’ani na kuzisambaza kwa duara ndogo ya jamaa na marafiki.
Aliongeza kuwa taasisi hiyo ilijaribu kwa miaka kadhaa kupata haki za uchapishaji wa tafsiri hiyo kutoka kwa mchapishaji wa Kiswidi aliyekuwa anazimiliki, lakini gharama yake ilikuwa kubwa mno.
Ataullah alieleza kwamba hatimaye mradi huo uliweza kununua haki hizo kwa msaada wa michango ya kifedha, ambapo mmoja wa wafadhili wa mwanzo alikuwa mwanasoka maarufu aliyetoa zaidi ya kronor 100,000 za Uswidi, huku akiomba jina lake lisitajwe.
Tafsiri ya Qur’ani kwa Kiswidi imechapishwa katika Kituo cha Nasyrul Quran kilichopo Putrajaya, Malaysia, ambacho ni miongoni mwa vituo vikubwa zaidi duniani vinavyobobea katika uchapishaji wa Qur’ani Tukufu.
Kituo cha Nasyrul Quran ni sehemu ya mpango wa kimataifa wa Malaysia wa kuchapisha na kusambaza nakala milioni moja za Qur’ani Tukufu katika zaidi ya lugha 50 duniani.
Kwa mujibu wa maafisa wa mradi huo, nakala 20,000 zitatengwa kwa Uswidi ili zisambazwe katika misikiti, taasisi na kwa wananchi kote nchini.
Sakina Förlag ndiyo itakayokuwa na jukumu la uchapishaji wa ndani, uhakiki wa ubora pamoja na usambazaji nchini Uswidi.
Maafisa wa utekelezaji wa mradi huo wanasema lengo kuu ni kueneza ujumbe wa jumla wa Uislamu, kuhamasisha watu kusoma Qur’ani mara kwa mara, na kuwapatia wazungumzaji wa Kiswidi tafsiri itakayowasaidia kuelewa vyema maana zake.
Tafsiri hii ya Qur’ani kwa Kiswidi imefanywa na Mohammed Knut Bernström, aliyewahi kuwa Balozi wa Uswidi nchini Morocco kati ya mwaka 1976 na 1983. Baada ya kusilimu na kuingia katika Uislamu, alichukua jina la Mohammed na ndipo akaanza kazi ya kuitafsiri Qur’ani Tukufu.
Bernström anajulikana kama mwandishi wa mojawapo ya tafsiri mashuhuri zaidi za Qur’ani kwa Kiswidi, iliyochapishwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwa miaka ya 1990 kwa jina “Koranens Budskap”, yaani “Ujumbe wa Qur’ani.”
3497499