IQNA

Spika wa Bunge la Uganda ataka vijana Waislamu wapate mafunzo ya sayansi

20:43 - February 20, 2014
Habari ID: 1377673
Spika wa Bunge la Uganda ametoa wito kwa nchi za Kiislamu kuzingatia zaidi suala la malezi ya vijana hasa wale ambao wanajihusisha na shughuli za kisayansi na kiufundi.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA, Bi. Rebecca Kadaga aliyasema hayo Jumatano mjini Tehran wakati akihutubia Kongamano la tisa la Jumuiya ya Mabunge ya Nchi za Kiislamu. Spika wa Bunge la Uganda amesema suala la teknolojia za kisasa linapaswa kupewa umuhimu mkubwa na nchi za Kiislamu kwani vijana wakipata mafunzo yanayofaa  katika uga wa sayansi wataweza kutatua matatizo mengi ya nchi zao.
Wakati  huo huo, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, yaani Bunge la Iran, amesema  bunge linaunga mkono ustawishwaji uhusiano baina ya Iran na Uganda.
Ali Larijani aliyasema hayo leo mjini Tehran wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Uganda Bi. Rebecca Kadaga. Spika huyo wa Bunge la Uganda akiwa na ujumbe wa wabunge kadhaa alikuwa Iran kuhudhuria Mkutano wa Tisa wa Jumuiya ya Mabunge ya Nchi za Kiislamu. Katika mkutano huo Larijani amesema Uganda imekuwa na nafasi muhimu katika kufanikisha malengo ya jumuiya hiyo.
Naye Spika wa Bunge la Uganda ameelezea furaha yake kushiriki katika mkutano wa mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na kuongeza kuwa uenyekiti wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika jumuiya hiyo ni jambo litakalopelekea kuimarika mshikamano wa nchi za Kiislamu.
Wakati huo huo maspika wa mabunge ya Kiislamu leo wametangaza uungaji mkono wao kamili kwa watu wa Palestina ambao wanakandamizwa na utawala haramu wa Israel. Akizungumza katika kikao hicho, Larijani ameelezea matumaini yake kuwa mabunge ya nchi za Kiislamu yatachukua hatua za kivitendo kutatua matatizo ya Wapalestina wanaodhulumiwa.
1377378

captcha