Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA, akizungumza kwa njia ya televisheni hapo jana, Sayyid Hassan Nasrullah amesisitiza kuwa, kama makundi ya kitakfiri na kigaidi yangelipata ushindi nchini Syria, asingelibakia mtu au harakati yoyote nchini Lebanon. Sayyid Nasrullah ameongeza kuwa wanamapambano wa Hizbullah waliingia nchini Syria yapata mwaka mmoja na nusu uliopita, wakati ambao makundi ya kigaidi yalikuwa yamebakisha mita 200 tu kulifikia kaburi la Bibi Zainab bint Ali (as) mjukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kuwa, kaburi la Bibi Zainab (as) linaheshimiwa na Waislamu wote wa Madhehebu ya Kishia na Kisuni duniani. Sayyid Hassan Nasrullah ameongeza kuwa, wakati vilipoanza vita vya Syria, Hizbullah ilipendekeza kutatuliwa mgogoro wa nchi hiyo kwa njia za kisiasa, lakini harakati hiyo ilibadilisha msimamo huo baada ya kuziona nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zikifadhilisha njia za kijeshi kuliko za kisiasa.