Hii ni katika hali ambayo tokea siku chache zilizopita utawala huo wa kibaguzi umekuwa ukifanya mashambulio makali ya anga katika ukanda huo ambapo raia wengi wasio hatia wa Kipalestina wameua na kujeruhiwa katika hujuma hiyo ya kinyama. Utawala huo umeamua kuanzisha mashambulio ya ardhini dhidi ya wakazi wa Gaza katika hali ambayo juhudi za kieneo na kimataifa zilikuwa zikiendelea kwa shabaha ya kusitisha vita baina ya jeshi la utawala huo na makundi ya mapambao ya Kipalestina, juhudi ambazo zilikuwa zimeanza kuzaa matunda kwa kutekelezwa usitishaji vita wa muda. Hata hivyo utawala unaopenda vita wa Israel uliamua kuvuruga juhudi hizo kwa kuanzisha mashambulio ya ardhini dhidi ya wakazi wa Gaza na hivyo kuvunja usitishaji vita huo uliokuwa umedumu kwa masaa machache tu. Kwa hivyo ni wazi kuwa kwa mara nyingine tena utawala haramu wa Israel umeamua kuanzisha hujuma nyingine kali dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza kupitia mashambulio ya kinyama ya ardhini, baharini na angani. Hayo yote yanafanyika katika hali ambayo jamii ya kimataifa imekaa kimya na kutazama tu raia wasio na hatia na hasa wanawake na watoto wa Palestina wakiuawa kinyama kwa mabomu ya Wazayuni. Kimya hicho kinathibitisha wazi kuwa mashambulio hayo ya kinyama dhidi ya raia wasio na ulinzi yanafanyika kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani kwa utawala huo haramu. Hii ndio maana John Kerry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, mara tu baada ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Isael kutoa amri ya kushambuliwa Gaza akasema kuwa hujuma hiyo inafanywa na utawala huo kwa lengo la kujilinda. Ni wazi kuwa uungaji mkono huo na vilevile uzembe wa jamii ya kimataifa katika kukabiliana na jinai za utawala wa Tel Aviv ndio umeupelekea utawala huo kuzidisha jinai zake dhidi ya Wapalestina wasio na hatia licha ya kuwepo malalamiko makubwa ya fikra za waliowengi duniani dhidi ya utawala huo. Kwa vyovyote vile hatua hizo za utawala wa Kizayuni zinathibitisha wazi kuwa utawala huo hautambui sheria zozote za kimataifa katika kufikia malengo yake ya kijinai dhidi ya Wapalestina. Lengo jingine la utawala haramu wa Israel kuanzisha hujuma ya nchi kavu huko Gaza ni kujaribu kufunika fedheha ya kushindwa kwake katika medani ya vita na makundi ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina ambayo katika siku za hivi karibuni yamevurumisha makombora katika vituo muhimu vya Wazayuni baada ya kushambuliwa na jeshi la Israel. Badhi ya wataalamu wa mambo ya Mashariki ya Kati wanaitakidi kwamba utawala wa Israel umeanzisha mashambulio ya ardhini huko Gaza ukiwa na ndoto ya kutaka kuukalia tena kwa mabavu ukanda huo. Awali Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas iliuonya utawala huo kuwa utalipa gharama kubwa kabla ya kufikia lengo hilo. Tayari wapiganaji wa makundi ya mapambano ya Kiislamu wamekabiliana vilivyo na hujuma hii mpya ya jeshi la utawala ghasibu wa Israel, jambo linaloonyesha kuwa utawala huo kwa mara nyingine tena unakaribia kufedheheshwa na Wapelestina wasio na silaha zozote za maana.