Sayyid Nasrullah amesema kuwa, muqawama ndiyo njia pekee inatakayoweza kuulazimisha utawala haramau wa Kizayuni kusitisha mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya Wapalestina. Alisema hayo jana katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds, iliyoadhimishwa duniani kote na kuongeza kama ninavyomnukuu: "Hii leo tunaona mafanikio makubwa ya muqawama huko Ghaza na kushindwa utawala wa Kizayuni katika kufikia malengo yake ya vita dhidi ya eneo hilo. Hii leo Ghaza inatoa ujumbe kwa adui Mzayuni kwamba, ikiwa mtakabiliana na wanamapambano wetu, basi mtaangamia na kushindwa." Mwisho wa kunukuu. Ameongeza kuwa, hii ni mara ya kwanza ambapo makombora ya wanamuqawama wa Kipalestina yanashambulia maeneo yote ya Wazayuni ukiwemo mji mkuu wa utawala huo Tel Aviv kutokea ndani ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kwamba hayo ni mafanikio makubwa sana. Amesisitiza kuwa, Hizbullah iko bega kwa bega na muqawama na Wapalestina kwa ujumla, lengo kuu likiwa ni kuondolewa mzingiro kwa eneo la Ghaza, kuwasaidia wanamapambano na mambo mengineyo. Aidha Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ametaka kuweka pembeni tofauti mbalimbali ili kuinusuru Ghaza. Ameongeza kuwa, Hizbullah inafuatilia kwa karibu matukio yanayojiri katika eneo hilo, kisiasa na katika medani ya mashambulizi na kwamba, muqawama ndio utakaoibuka mshindi. Vile vile amesema kuwa, kwa miaka mingi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Syria na muqawama wa Hizbullah zimekuwa zikiunga mkono mapambano ya wananchi wa Palestina, kisiasa, kisilaha na kistratijia. Akikumbushia matukio ya vita ya siku 33 mwaka 2006, kati ya harakati ya Hizbullah na utawala katili wa Kizayuni, Sayyid Hassan amesema kuwa, Lebanon ilitoa watu wengi waliouawa shahidi katika njia ya haki lakini mwisho wa yote, ilikuwa ni kupatikana ushindi wa kimiujiza na kuogeza kuwa, Walebanon wanafahamu vyema kinachowapata hivi sasa wakazi wa Ghaza kwa sababu ndiyo yale yale yaliyowapata wao mwaka 2006.
1433213