IQNA

Kadhia ya Palestina

Hamas yalaani hatua ya DRC kuamua kuhamishia ubalozi wake Al Quds

13:06 - September 24, 2023
Habari ID: 3477647
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani uamuzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Al Quds inayokaliwa kwa mabavu (Jerusalem) na kutaka kuangaliwa upya uamuzi huo.

Ni baada ya Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu kudai kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itahamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Al-Quds (Jerusalem).

Katika taarifa yake, harakati ya Hamas imelaani uamuzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuhamishia ubalozi wake huko Quds inayokaliwa kwa mabavu na imetambua uamuzi huo kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Taarifa ya Hamas pia imetangaza kwamba hatua hiyo ina maana ya kukanyaga haki za watu wa Palestina katika mji mkuu wa kihistoria na nembo yake ya kidini na kisiasa.

Taarifa ya harakati hiyo ya kupigania ukombozi wa Palestina  imeitaka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutupilia mbali uamuzi huo.

Waziri Mkuu wa Israel,  Benjami Netanyahu alidokeza Ijumaa iliyopita baada ya kukutana na Rais wa DRC, Félix-Antoine Tshisekedi pambizoni mwa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New  York kwamba Congo imekubali kuhamishia ubalozi wake Quds inayokaliwa kwa mabavu.

Netanyahu aliongeza kuwa, utawala huo haramu unaokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina karibuni hivi utafungua ubalozi wake huko Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

4170755

Kishikizo: ubalozi quds palestina
captcha