Tahafifu hiyo iliyotangazwa leo na Mufti Mkuu wa Misri imewajumuisha pia washtakiwa wengine watano ambao kama Badie walihukumiwa pia adhabu ya kifo na mahakama ya Misri. Kiongozi huyo Mkuu wa Ikhwanul Muslimin na wenzake hao walihukumiwa adhabu ya kifo tarehe 19 Juni mwaka huu wakidaiwa kuhusika na mauaji ya maafisa wa polisi wakati wa maandamano ya upinzani, lakini Mufti Mkuu wa Misri alikataa kuidhinisha hukumu hiyo. Katika hatua isiyo ya kawaida waendesha mashtaka katika kesi hiyo walimtaka kiongozi huyo mwenye mamlaka ya juu kabisa ya kidini nchini Misri afikirie tena uamuzi wake huo. Mbali na kesi hiyo, Mohamed Badie tayari alishahukumiwa adhabu ya kifo katika kesi nyengine pamoja na wanachama na wafuasi wengine 182 wa harakati ya Ikhwanul Muslimin, hukumu ambayo imeamsha hasira za makundi ya kutetea haki za binadamu.