IQNA

Wafanya ziara kutoka zaidi ya nchi 60 katika Arubaini huko Kabala

17:46 - December 13, 2014
Habari ID: 2617895
Takribani watu milioni 20 wamewasili Karbala kwa ajili ya kushiriki katika Arubaini ya Imam Husain AS. Mkuu huyo wa mkoa wa Karbala amesema kuwa hii ni mara ya kwanza kabisa kumiminika watu kiasi chote hicho katika historia ya ziara za Imam Husain AS.

Inafaa kusema hapa kuwa, watu kutoka nchi 60 tofauti za dunia wamemiminika huko Karbla Iraq kwa ajili ya kufanya ziara na kushiriki katika Arubaini ya Imam Husain AS. Idadi kubwa zaidi ya wafanya ziara hao wanatoka katika nchi za Iran, Kuwait, Saudi Arabia, Bahrain, Jordan, Syria, Algeria, Tunisia na Misri. Viongozi wa Iraq wamesema kuwa, idadi ya wafanya ziara itaongezeka leo Jumamosi ambapo ndiyo siku ya Arubaini ya Imam Husain AS. Kwa upande wake, Wizara ya Ulinzi ya Iraq imetoa taarifa na kusema kuwa, imevunja jaribio la kigaidi dhidi ya wafanya ziara hao wa Arubaini ya Imam Husain AS. Wizara hiyo imetangaza kuwa, maafisa usalama wa kitengo cha Furat jana Ijumaa waligundua maeneo 16 yaliyokuwa yamefichwa katika vilima vya at Tar vikiwa tayari kwa ajili ya kuvurumisha maroketi. Mkuu wa kamati ya usalama katika Baraza la Mkoa wa Babil, Bw. Fallah al Khaffaji naye amesema kuwa, mpango maalumu wa usalama kwa ajili ya kuimarisha ulinzi katika Arubaini ya Imam Husain AS unaendelea vizuri kwa ushirikiano wa kupigiwa mfano wa wananchi, wafanya ziara na maafisa usalama wa Iraq. Ameongeza kuwa, maafisa usalama wamemaliza vizuri sehemu ya kwanza ya mpango huo na wameimarisha vizuri ulinzi wa kuingia Karbala wafanya ziara hao. Amesema, hatua ya pili ya mpango huo ni kulinda usalama wa wafanya ziara hao wakati watakapoondoka Karbla na kurejea makwao. Kwa upande wake, mwakilishi wa marjaa wa kidini wa Iraq amewashukuru wale wote ambao hadi hivi sasa wameshiriki katika ufanikishaji wa Arubaini ya Imam Husain AS. Amma jambo la kuvutia zaidi katika maadhimisho ya mwaka huu ya Arubaini ya Imam Husain AS ni kushiriki kwa wingi zaidi Waislamu wa Kisuni katika maadhimisho hayo kutoka mikoa mbalimbali ya Iraq huku wakisisitizia umuhimu wa mshikamano na kuwa kitu kimoja wananchi wa nchi hiyo. Ujumbe wa watu wazito wa kikabila na kidini wa Waislamu wa Kisuni kutoka mikoa ya Salahuddin, Nainawa, al Anbar na Baghdad jana Ijumaa uliwasili Karbala kwa ajili ya kuonyesha umoja na mshikamano wao na Waislamu wenzao wa Kishia wakisisitiza kuwa wananchi wote wa Iraq wako pamoja katika kupambana na makundi ya kigaidi na kitakfiri kama vile Daesh. Hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wa kidini wa Kishia wa Iraq kutoa fatwa katika miezi ya hivi karibuni, ya kujitokeza Wairaqi wote kuilinda nchi yao mbele ya mashambulizi ya magaidi, bila ya kujali tofauti zao za kimadhehebu. Waislamu wengi wa Kishia wameitikia vilivyo mwito huo na hivi sasa wanapambana bega kwa bega na ndugu zao wa Kisuni katika mapambano dhidi ya magaidi wa Daesh kwenye mikoa kama ya Salahuddin, Nainawa, al Anbar, Diyala, Kirkuk na Mosul. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Bw. Haydar al Aaraji, mmoja wa wakuu wa kikabila wa mkoa wa Nainawa akasema alipofika Karbala kuwa, ujumbe wa viongozi wa kikabila wa Kisuni kwa magaidi wa Daesh ni kwamba njama za magaidi hao za kuisambaratisha Iraq zitashindwa na Wairaq wote wataendelea kuishi pamoja kwa amani bila ya kujali dini na madhehebu yao. Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo pia ndio maana Arubaini ya Imam Husain AS mwaka huu ikafanyika kwa kufana zaidi na kushirikisha idadi kubwa zaidi ya Waislamu wa madhehebu tofauti. Kuimarishwa ulinzi kwa ajili ya wafanyaziara nako kunaonesha ni kiasi gani wananchi wa Iraq wanavyoweza kusimamia wenyewe usalama wa nchi yao bila ya kuhitajia uingiliaji wa madola ya kigeni.../mh

2617751

captcha