Hayo yamo katika mahojiano aliyofanyiwa mchambuzi maarufu wa masuala ya kisiasa wa nchini Marekani, Mark Glenn na televisheni ya Press TV. Amesema : "Mimi nadhani wapinzani wa Syria kimsingi wako katika siku zao za mwisho. Fedha na miongozo waliyokuwa wakipata kutoka kwa Marekani na duru nyinginezo, kimsingi zimeondolewa na ndio maana hivi sasa tunawaona wapinzani hao wakielemewa." Vile vile amesema kuwa, hasara zilizosababishwa na makundi ya wanamgambo huko Syria hazikadiriki. Amesema pamoja na hali kuwa hivyo lakini huu si wakati wa kulaumiana kuhusu mgogoro wa miaka mitatu sasa nchini Syria. Aidha mchambuzi huyo maarufu wa masuala ya kisiasa wa nchini Marekani, ameilaumu Saudi Arabia kwa kuchochea machafuko nchini Syria kwa niaba ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Huku hayo yakiripotiwa, habari zinasema kuwa magenge ya kigaidi yanaendelea kupigana yenyewe kwa yenywe nchini Syria ambapo jana Jumamosi wanamgambo 36 wa al Qaida waliuliwa na kundi jingine la waasi lililozuka hivi karibuni nchini Syria.../mh