IQNA

Kiongozi Muadhamu: Saudia imefanya kosa kubwa kuivamia Yemen

11:01 - May 14, 2015
Habari ID: 3300744
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Saudi Arabia imefanya kosa kubwa la kuivamia na kuishambulia kinyama Yemen na bila ya shaka yoyote madhara ya jinai wanazofanya huko Yemen yatawarejea wenyewe.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo siku ya Jumatano jioni mjini Tehran katika mazungumzo yake na Rais Fuad Ma'asum wa Iraq pamoja na ujumbe alioandamana nao.
Ametaka mashambulio na mauaji dhidi ya wananchi wa Yemen yakomeshwe mara moja na kuongeza kwamba, fikra isiyo ya busara na ya kijahili ndani ya serikali ya Saudia ndiyo inayochukua maamuzi kuhusiana na Yemen.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja njama za maadui wa Uislamu dhidi ya Syria kuwa ni hatari kubwa sana na kusisitiza kwamba, maadui wana nia ya kueneza vurugu na kuhakikisha kuwa ukosefu wa amani unadumu nchini Syria ili kulifanya eneo hili zima lisiwe na utulivu.
Ayatullahil Udhma Khamenei amegusia pia hali ya kusikitisha ya nchini Yemen na kusisitiza kuwa, Wasaudia wamefanya kosa kubwa la kuivamia na kuishambulia kinyama Yemen na bila ya shaka yoyote madhara ya jinai wanazofanya huko Yemen yatawarejea wenyewe.
Kwingineko katika matamshi yake ameitaja Iraq kuwa, nchi hiyo ni yenye taathira katika masuala ya eneo la Mashariki ya Kati kutokana na umuhimu na nafasi yake ya kipekee.
Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa Iraq inaweza kuwa na taathira kubwa katika nchi za Kiarabu na za Kiislamu na inabidi uwezo na nafasi hiyo itumiwe vizuri kadiri inavyowezekana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq ni mkubwa na ni wa kina na amekaribisha juhudi za kupanua uhusiano wa nchi hizo mbili kadiri inavyowezekana. Aidha amesema, uhusiano wa hivi sasa wa Iran na Iraq ni wa kipekee kabisa ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma.
Katika mazungumzo hayo ambayo yamehudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Fuad Ma'asum wa Iraq kwa mara nyingine tena ameishukuru Iran kwa kuwasaidia wananchi na serikali ya nchi yake katika wakati mgumu kabisa wa uvamizi wa kundi la kigaidi la Daesh na kuongeza kuwa, Daesh ya Iraq na Daesh ya Syria hazina tofauti yoyote kwani kundi hilo la kigaidi ni hatari kwa watu wote..../mh

3299695

captcha