IQNA

Wito wa kushtakiwa walioshambulia Ofisi ya Ayatullah Sistani nchini Syria

16:25 - June 07, 2025
Habari ID: 3480801
IQNA – Khatibu wa Swala ya Ijumaa jijini Baghdad amesisitiza umuhimu wa kuwachukulia hatua kali waliotekeleza shambulizi dhidi ya ofisi ya Ayatullah Ali Sistani mjini Damascus, mji mkuu wa Syria.

Katika hotuba yake ya Swala ya Ijumaa, Sayyid Sadreddin Qabanchi amesema kuwa Ayatullah Sistani, kiongozi mkuu wa kidini yaani Marjaa Taqlid, ni mtu mashuhuri na mwenye heshima kubwa miongoni mwa Waislamu wa Kishia na hata wa madhehebu mengine.
"Shambulizi dhidi ya ofisi ya Ayatullah Sistani ni hujuma dhidi ya moja ya nguzo kuu za jamii yetu ya Kiislamu, jambo ambalo hatuwezi kuvumilia," alisisitiza.
"Tunasubiri kuona wahusika wakichukuliwa hatua stahiki; kuomba msamaha pekee hakutoshi."

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Qabanchi amewashukuru maafisa wa usalama wa Iraq kwa mafanikio yao ya kuwakamata wanachama wa chama cha Baath waliokuwa wakikutana mjini Sulaymaniyah, wakiwemo jamaa wa karibu wa aliyekuwa dikteta wa Iraq, Saddam Hussein.
Amesema kuwa hiyo ni hatua kubwa na ya kishujaa, kwani vikosi vya usalama vilifanikiwa kubaini muda na eneo la kikao hicho, na kuchukua hatua kwa haraka.

Mapema wiki hii, wakuu wa wanamgambo waliovamia ofisi ya Ayatullah Sistani katika mtaa wa Sayyidah Zaynab, kusini mwa Damascus, waliomba radhi rasmi kwa kitendo chao.

Kwa mujibu wa Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu la Syria, shambulizi hilo lilitokea Jumanne na lilitekelezwa na kundi lenye itikadi kali linaloongozwa na mtu anayeitwa Abu Omar al-Libi.
Ofisi hiyo iliharibiwa vibaya – milango, nguzo za ndani, na mali nyingine ziliibwa.

Vyanzo vya karibu na ofisi hiyo vilieleza kuwa shughuli zake ni za kibinadamu tu ,ikijikita zaidi katika kuhudumia mayatima na kuwasaidia Waislamu wa Kishia waliolazimika kuhama , bila ushiriki wowote wa kijeshi au kisiasa.
Baada ya mazungumzo na upatanisho, baadhi ya mali zilizoibwa zilirudishwa na kundi hilo likatoa msamaha rasmi.

3493347

captcha