Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, fainali ya mashindano hayo imefanyika Alkhamisi ambapo katika kitengo cha kuhifadhi kikamilifu Qur'ani Tukufu, Sheikh Mohammad Mehdi Rajabi wa Iran amechukua nafasi ya kwanza akifuatiwa na Abdullah Ar Rafai kutoka Libya na nafasi ya tatu ikishikwa na Hassan Asaka wa Niger naye Abubakr Musa wa Uganda amechukua nafasi ya nne ambapo Adam Hassan wa Somalia ameweza kuibuka wa tano.
Katika kitengo cha qiraa au kusoma Qur'ani Tukufu kwa tajwidi, nafasi ya kwanza imechukuliwa na Hassan Danesh wa Iran akifuatiwa na Mohammad Abdul Basit Mohammad Abdul Rahman wa Misri. Mohammad Ibrahim wa Pakistan amepata nafasi ya tatu naye Ja'afar Hasibuan wa Indonesia ameshika nafasi ya nne huku Ahmad Abbas Faraj wa Iraq akiwa wa tano.
Mashindano hayo yalianza Ijumaa iliyopita na yamekuwa yakiendelea kila siku ambapo kulikuwa na washiriki 120 kutoka nchi 75 duniani.
Sherehe za kufunga rasmi Awamu ya 32 ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran zitafanyika leo Ijumaa alasiri na kuhudhuriwa na Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, katika Ukumbi wa Mkutano wa Nchi za Kiislamu hapa Tehran. Walioshika nafasi za tano za kwanza katika vitengo vyote viwili vya hifdhi na qiraa watatunukiwa zawadi.../mh