IQNA

Maandamano ya amani Tanzania kuwaunga mkono Wapalestina

1:14 - July 03, 2015
Habari ID: 3322431
Jumuiya ya Waislamu wa Kishia Tanzania, AfroShia Muslim Community, inapanga maandamano ya amani kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds kwa lengo la kulaani jinai dhidi ya Wapalestina na pia kuunga mkono jitihada za amani duniani.

Kiongozi wa jumuiya hiyo Sheikh Hemedi Jalala ametoa tangaza hilo  hivi karibuni katika warsha maalaumu ya wahubiri wa Kiislamu iliyoitishwa kujadili kadhia ya Palestina. Washiriki katika warsha hiyo walitathmini njia muafaka za kurejesha amani Palestina.
Sheikh Jalala ametoa wito kwa Waislamu na Watanzania kwa jumla kulaani jinai za utawala haramu wa Israel huko Palestina. Aidha amewataka kuombea amani irejee katika taifa hilo linalodhulumiwa.
Sheikh Jalala ameongeza kuwa Watanzania wanapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajali ya amani iliyo katika nchi yao. Hatahivyo aliongeza kuwa, kuwepo na amani hakutoshi iwapo wanaadamu katika maeneo mengine wanaishi katika hali ya ukosefu wa amani. Kiongozi huyo wa Mashia nchini Tanzania ameongeza kuwa: ‘Palestina inapaswa kuwa huru na kukombolewa kutoka mateso, ubaguzi, mauaji na dhulma zingine inazotendewa kwani wakaazi wake wanahitaji amani. Maandamano tuliyoitisha yanalenga kuombea amani kwa ajli ya Palestina na dunia nzima.’
Maandamano hayo ya amani kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds yamepangwa kufanyika Ijumaa Julai 10 mjini Dar es Salaam.
Siku ya Quds huadhimishwa kote duniani katika Ijumaa ya Mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo Waislamu na wapenda haki kote duniani hujitokeza katika maadamano ya amani kuunga mkono harakati za ukombozi wa Palestina sambamba na kulaani jinai za utawala haramu wa Israel.
Hivi karibuni Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilitoa taarifa na kulaani namna Israel ilivyoendesha vita dhidi ya Ghaza mwaka jana.
Taarifa ya tume hiyo ilisema Israel ilikuka sheria za kimataifa katika vita vyake dhidi ya Ghaza. Aidha Mamlaka ya Ndani  ya Palestina imikabidhi Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC faili kadhaa zenye ushahidi wa jinai za kivita zilizotendwa na Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza. Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo Bi. Fatou Bensouda amesema mahakama hiyo imeanza kufanya uchunguzi kuhusu jinai za Israel dhidi ya Wapalestina.../mh

3322162

captcha