IQNA

Sheikh wa Al Azhar apinga kukufurishwa Mashia

19:25 - July 04, 2015
Habari ID: 3323156
Shekhe Mkuu wa Chuo Kikuu cha kidini cha al Azhar nchini Misri amepinga hatua ya wahubiri wa Kiwahabi na Kisalafi ya kutumia kauli isiyofaa ya ‘Rafidh’ kuwataja Wapenzi wa Ahul Bayt wa Mtume SAW.

Kwa mujibu wa tovuti ya al Yawm al Sabi, Sheikh Mkuu wa al Azhar, Ahmad Tayyib katika hotuba aliyoitoa kwenye kanali ya televisheni ya Misri hivi karibuni, amekosoa na kupinga kutumika neno Rafidh kuwahutubu Waislamu wa madhehebu ya Shia na wapenzi au muhibina wa Ahul Bayt watoharifu. Sheikh Ahmad Tayyib ameongeza kuwa al Azhar si taasisi ya kueneza fitna na mifarakano baina ya Waislamu. Mwanachuoni huyo mkubwa nchini Misri amesisitiza kuwa, al Azhar ni taasisi yenye lengo la kutafuta njia za kuleta umoja katika umma wa Kiislamu. Sheikh Mkuu wa al Azhar amesema, katika karne iliyopita, taasisi hiyo imekuwa ikiongoza mikakati ya kuleta maelewano baina ya Waislamu wa Kisunni na Kishia na daima imekuwa ikifuatilia kadhia ya umoja wa Waislamu. Ameongeza kuwa matatizo mengi ya Waislamu leo yanatokana na kukosekana umoja na kuweko mifarakano baina ya Mashia na Masunni. Sheikh Ahmad Tayyib ameashiria madai yasiyo na msingi yanayotolewa dhidi ya Mashia na kusema, ‘suala la kuwakufurisha Mashia na Wapenzi wa Ahul Bayt wa Mtume SAW ni kati ya mambo yanayoleta uhasama miongoni mwa Waislamu. Amesema haijuzu kisheria na haifai kuwaita Mashia kuwa ni Rafidh. Mkuu wa Chuo Kikuu cha al Azhar ametoa mwito kwa maulamaa wa Kishia na Kisunni ambao wanajali mustakabali wa umma wa Kiislamu kuchukua hatua za kusaidia kusitisha mauaji na uharibifu katika umma wa Kiislamu.../mh

3322878

captcha