Sayyid al-Huthi aliyasema hayo jana jioni katika hotuba aliyoitoa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds, iliyoadhimishwa kote duniani katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Amesema kuwa, ni baada ya raia wa Yemen kuchagua kuwa pamoja na muqawama wa Palestina na Lebanon katika kukabiliana na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ndio maana wanashambuliwa kila upande na maadui.
Kiongozi wa Ansarullah amewataka Wayemen kwa ujumla kujiandaa kwa chaguo kubwa la kistratijia, ikiwa mashambulizi ya kichokozi yanayofanywa na Saudia na waitifaki wake, hayatakoma nchini humo. Aidha Abdul-Malik al-Huthi, ametaka kuzibwa pengo la utawala na Wayemene wenyewe bila kusubiri msaada kutoka nje na kusisitiza kuwa, ikiwa hujuma hizo hazitasitishwa, basi harakati hiyo haitakuwa na budi ghairi ya kufuata chaguo hilo la dharura katika kukabiliana na chokochoko hizo. Akiashiria mpango wa usitishaji wa muda wa mashambulio hayo, amesema kuwa Wayemen hawana matarajio kuwa usitishaji huo wa muda utaweza kuwa na mafanikio na kuongeza kuwa, mafanikio ya mpango huo yanaweza kufikiwa ikiwa upande wa pili utatekeleza masharti ya makubaliano.
Saudi Arabia ilianza kuishambulia kijeshi Yemen tangu tarehe 26 Machi, na hadi sasa watu zaidi ya 4,600 wameshauawa wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto. Aidha ndege za kivita za Saudia zimedondosha mabomu katika misikiti, shule, hospitali, madaraja n.k.
Saudia imekaidi ombi la Umoja wa Mataifa la kusitisha hujuma dhidi ya watu wa Yemen katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.../mh