IQNA

Ustadh Tarouti wa Misri aomboleza vifo vya maqarii Wairani Mina

11:50 - September 27, 2015
Habari ID: 3372198
Qarii mashuhuri na mtajika wa Misri, Ustadh Dkt. Abdul Fattah Tarouti ametuma salamu zake za rambi rambi kufuatia kurejea kwa Mola wao maqarii hao wawili wa kimataifa waliokuwa wakitekeleza ibada ya Hija katika eneo la Mina karibu na mji mtakatifu wa Makkah.

Dkt. Tarouti ambaye alikuwa jaji katika Mashindano ya 57 ya Kimatiafa ya Qur’ani Malaysia mwezi Juni, ambapo qarii Muirani aliyeaga dunia Mina Mohsen Hajihassani Kargar  alichukua nafasi ya kwanza, katika ujumbe maalumu uliopokewa na IQNA amesema amepata huzni na majonzi kufuatia kifo cha qarii huyo Muirani.
Katika ujumbe wake Ustadh Tartouti amesema: "Nimeumia moyo kwa kuwa, wakati nimetimiza faradhi ya Hija na nilipokuwa nikirejea nyumbani nilipokea habari kuwa Mohsen Hajihassani Kargar ameitikia mwito wa Mola wake kwa kutamka Labbayk na kurejea mbele ya haki. Nilikuwa takribani mita 300 kutoka eneo la tukio na wala sikudhani Mohsen, azizi wangu, alikuwa miongoni mwa mashahidi. Kwa baraka ya Qur'ani anaelekea peponi."


Akizihutubu familia za maqarii wa Qur'ani waliokufa shahidi Mina, Ustadh Tarouti amesema: "Hampaswi kuomboleza bali kwa hakika mnastahiki pongezi kwa fadhila na karama za Allah SWT. Hii ni kwa sababu mashahidi wenu wa Qur'ani wameitikia mwito wa Allah SWT na kutamka Labbayk naye Allah SWT akawachukua waja wake hao wakiwa katika hali ya kuwa wamevalia vazi la Ihramu."


Ikumbukwe kuwa  Alhamisi iliyopita mahujaji takribani 2,000  wakiwemo Wairani 136 wamethibitishwa kupoteza maisha katika maafa ya Mina. Miongoni mwa waliopoteza maisha walikuwemo maqarii wawili wa kimataifa wa Iran, Mohsen Hajihassani Kargar na Amin Bavi.../mh

3372099

captcha